NSSF yaweka wazi matokeo chanya

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema, kati ya Machi Mosi, 2021 na Juni 30, 2023, waliandikisha jumla ya wanachama 547,882 ambapo idadi ya wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36.

Ni kutoka 874,082 Machi Mosi, 2021 hadi kufikia wanachama 1,189,222 Juni 30, 2023 ikichangiwa na mkakati wa Serikali wa kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa mfuko katika uandikishaji wanachama.

Hayo yamesemwa leo Septemba 25, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba katika kikoa kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Leo, hii ni taasisi ya 16 kati ya taasisi na mashirika yaliyopo chini ya Msajili wa Ofisi ya Hazina ambapo Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ameyaelekeza kukutana na wahariri ili kueleza umma yalipotoka, yalipo,yanapoelekea na mafanikio yake.

NSSF ulianzishwa mwaka 1964 kama kitengo ndani ya Wizara ya Kazi kinachoshughulikia mafao ya wafanyakazi baada ya kustaafu. Mwaka 1975,kitengo hicho kiliboreshwa na kuwa taasisi inayojitegemea iliyoitwa National Provident Fund (NPF).

Aidha, maboresho zaidi yalifanyika mwaka 1997, ambapo Sheria Na. 28 ilitungwa na kuibadili NPF kuwa Mfuko wa Pensheni, hivyo kuwezesha kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi.

Mwaka 2018 Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii yaliyosababisha kurekebishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50.

Uamuzi huo uliifanya NSSF kuwa mfuko pekee unaohudumia hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na wale wa sekta isiyo rasmi nchini.

Amesema,wanachama wachangiaji katika mfuko wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia wanachama wachangiaji 1,189,222 tarehe 30 Juni 2023 ikilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa tarehe 30 Juni 2021.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023,makusanyo ya michango kwa mwezi uliongezeka kutoka shilingi bilioni 97.67 iliyofikiwa Machi Mosi,2021 hadi kufikia shilingi bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2023.

“Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaoleta michango kwa wakati na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi.”

Aidha, Mshomba amesema,makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia shilingi bilioni 1,718.28 katika mwaka ulioishia Juni 30,2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 1,201.05 zilizokusanywa katika mwaka ulioishia Juni 30,2021.

Uwekezaji

“Uwekezaji wa Mfuko (investment portfolio) iliongezeka kwa asilimia 111 kutoka shilingi bilioni 3,395.46 tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023 ikichangiwa na kukua kwa thamani ya vitega uchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.”

Pia, amesema thamani ya vitega uchumi vya mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia shilingi bilioni 7,153.23 tarehe 30 Juni 2023 kutoka shilingi bilioni 4,622.25 zilizofikiwa tarehe 30 Juni 2021.

Mshomba ameendelea kufafanua kuwa, wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katikamwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023, yalifika shilingi bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na shilingi bilioni 37.35 zilizokusanywa mwezi Machi 2021.

Aidha, mapato halisi (real rate of return on investment) ya mfuko, amesema yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 mwezi Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2023.

“Mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia shilingi bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 30 Juni 2021.”

Vile vile amesema,katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023,mfuko ulilipa shilingi bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ukilinganisha na shilingi bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia tarehe 1 Machi 2021.

“Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) na mkupuo maalum (special lumpsum).”

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 na kufikia shilingi bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023 ukilinganisha na shilingi bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia tarehe 30 Juni 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news