Prof.Muhongo:Ujenzi David Massamba Memorial Sekondary School kuanza mwezi huu

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo amewaomba wananchi wa jimbo hilo wajiandae na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya David Massamba Memorial Sekondary School jimboni humo utakaoanza mwezi huu wa Septemba, 2023.

Ujenzi wa shule hiyo utafanyika kijijini kwao, na ni dhamira ya dhati ya wananchi wa jimbo hilo na Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo waliokubaliana katika kumuenzi nguli wa Lugha ya Kiswahili hapa nchini na nje ya Afrika, Prof. David Massamba aliyefariki dunia na kuzikwa Agosti 30,2023 nyumbani kwake kijijini Kurwaki Musoma Vijijini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo Septemba 1,2023 imeeleza kuwa,"Kumuenzi ni wajibu wetu. Tutajenga Sekondari yenye jina lake, David Massamba Memorial Secondary School." imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa,"ujenzi unaanza mwezi huu, Septemba 2023. Tujitayarishe kuchangia ujenzi wa sekondari hiyo."imesema taarifa hiyo.

Meshack Godfrey ni mkazi wa Kata ya Mugango Wilaya ya Musoma akiongea na DIRAMAKINI amesema kuwa, wamejiandaa na ujenzi huo ili kumuenzi Prof. David Massamba kwani alikuwa na mchango mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

"Kiswahili ni lugha yetu, tunaposema lugha ya kiswahili imekuwa na faida kubwa Sana katika mawasiliano ya nyanja mbalimbali ikiwemo biashara na kutuunganisha pamoja Watanzania. Prof. Massamba hatuwezi kumuweka kando nguli huyu wa Kiswahili,"amesema Fabian Juma mkazi wa Mugango na kuongeza kuwa.
 
"Prof. Massamba amefundisha watu wengi, pia amechangia kukikuza hadi nje ya mipaka yetu niwashukuru wananchi wa Musoma Vijijini na mbunge wetu Prof. Muhongo kwa kuamua tumuenzi kwa kujenga shule itakayoitwa jina lake huu ni uamuzi wa busara sana."

Aidha, wataalamu wenzake wa lugha ya Kiswahili, wakiwemo wanafunzi wake wanasema marehemu Prof. David Massamba alikuwa Gwiji na Mbobezi kwenye eneo la, "Fonolojia ya Kibantu" na hayupo mwingine tena wa kariba yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news