Rais Dkt.Mwinyi aendesha harambee kuchangia BBT

DAR ES SALAAM-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Husein Ali Mwinyi ameendesha harambee ya washirika mbalimbali kuchangia utekelezaji wa Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).

Harambee hiyo imefanyika Septemba 7, 2023 katika mkutano wa pembeni wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaoendelea kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, kumekuwa na utashi wa kisiasa unaokua kwa kasi barani Afrika hususani Tanzania unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake katika kilimo biashara.

Amesema, utashi huo unaonekana kufuatia juhudi mbalimbali ikiwemo kupitishwa mikataba ya tamko la mpango wa utekelezaji wa vijana, kunzishwa kwa dawati la vijana katika mpango mpya wa ushirikiano wa pamoja na uwezeshaji mpango wa BBT.

Pia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,Serikali imeandaa mikakati shirikishi na kutekeleza mipango ya kusaidia vijana na wanawake katika sekta ya kilimo biashara katika hatua za uwezeshaji wa mradi wa BBT utaongeza ajira kupitia mfumo wa chakula.

Amesema, kutokana na kukua kwa mifumo ya kidigitali inayosimamia mabadiliko ya uchumi wa dunia kumekuwa na ongezeko la kasi kwa vijana kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi Afrika kupitia kilimo.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi akizungumza kuhusiana na vijana amesema, vijana wana hamu ya kuwekeza sehemu zenye matokeo ya haraka.

Amesema, ili kufikia mafanikio yapo maeneo yanahitaji ufumbuzi ikiwemo upatikanaji wa huduma za kijamii vijijini hatua ambayo itasaidia kupunguza wimbi la vijana ambao wanao uwezo wa kushiriki katika kilimo kuhamia mjini.

“Pia ni muhimu kumaliza tatizo la kukosekana kwa masoko, vikwazo vya kimazingira na mabadilioo ya tabia nchi, kukosekana kwa miundombinu ya uzalishaji na kutafuta ufumbuzi katika uwekezaji wa teknolojia,”amebainisha Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Akizungumzia uwezeshaji wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo amesema, ufunguo wa milango ya ajira ni kilimo ambacho kinaweza kuwa chanzo cha kupunguza umaskini na matokeo ya uzalishaji wa chakula na kujiongezea thamani.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, ili kufikia malengo hayo,Serikali ya Tanzania imejizatiti katika kuwawezesha vijana na wanawake kufikia malengo yao, ikiwemo kuwepo kwa mazingira wezeshi katika kilimo biashara.

Naye Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe amesema, lengo la Serikali ni kukusanya zaidi ya dola bilioni mbili kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa BBT unaoisha mwaka 2030.

Bashe amesema, hatua hiyo itawezesha ukuaji wa uchumi kwa kuwa kilimo kinachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa huku asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo,pia kinatoa asilimia 75 ya ajira na kuchangia mauzo ya nje ya nchi kwa asilimia 85.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news