Salamu za Jumapili: SEMA MIMI NI HODARI

NA LWAGA MWAMBANDE

MONGONI mwa watumishi wa Mungu hapa nchini, Samson Ernest amewahi kuandika katika moja ya machapicho yake mtandaoni kuwa, kinywa kina nguvu.

Picha na eatthis.
 
Vivyo, hivyo kinywa kinaweza kunena jambo na likawa, liwe jema au liwe baya. Kile unakiri mara kwa mara, ndivyo utakavyokuwa.

Ukiri wa jambo unatokana na mazingira ya mtu alipo, sio kana kwamba mtu anakuwa mwongo vile ananena. Mara nyingi huwa tunanena maneno kutokana na hali tunazopitia, inaweza ikawa hali nzuri au mbaya.

Tunaposema hali ngumu, ni mazingira yanaonesha hivyo, sio kwamba tunadanganya, huenda ulipo una hali ngumu kweli. Pamoja na unaona hali ngumu, yupo mtu haoni huo ugumu, hata kama mpo pamoja.

Wakati mwingine sio kana kwamba yule anayeona hali nzuri, ni kwa sababu yeye yupo kwenye hali nzuri. Vile anachukulia mambo, vile anaona ushindi ulio mbele yake.

Mtu huyu anakuwa hasumbuliwi kabisa na kipindi kigumu anachopitia kwa muda huo, maana yeye anatazama lengo lake la kufikia ule uzuri anaouona kwenye maono yake.

Kwa hiyo hali yake ya sasa haimtishi sana, anahakikisha anaendelea kujiweka vizuri na Mungu wake, ili afikie yale malengo yake.

Mtu wa namna hiyo huwezi kumkuta anakiri udhaifu, huwezi kumkuta anakiri kushindwa, na huwezi kumkuta anaungana na marafiki zake waliokata tamaa na yeye awe miongoni mwao.

Ukimkuta yupo miongoni mwa kundi lililokata tamaa, ana kazi maalum kwenye hilo kundi, hata matendo yake ukiyatazama utaona yanaonyesha wazi kuwa ni mtu mwenye ukiri wa ushindi.

Umefika mahali umechoka, huna msukumo wowote wa kuendelea na kile Mungu alikupa ndani yako. Kuanzia sasa kiri ushindi, hata kama unaonekana kwa nje u dhaifu, elewa kwa Mungu haipo hivyo.

Picha gani unaiona kwenye kesho yako, ona una nguvu, ona u hodari, ona ushujaa. Kujiona hivyo utaanza kuona mabadiliko yakitokea ndani yako, utaanza kuona kushinda na sio kushindwa.

Mungu wetu ni mwaminifu, yupo pamoja nasi, hata katika hali duni, tukimwita, yeye atatushindia kwa yote.Rejea, Yoel 3:10...Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari."

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa bila kujali hali unayopitia wewe uliye dhaifu, kiri wewe ni hodari na songa mbele. Endelea;

1. Bila ya kujali hali, ujitamkie mema,
Kusema wala si ghali, ni mwenyewe kujituma,
Hali iwe ni dhalili, moyo wako kuinama,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

2. Hata kama ni dhaifu, si kujinenea mema,
Hali yako ikukifu, kama vile una homa,
Kiri na ujiarifu, ya kwamba utasimama,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

3. Ndivyo unavyoyaumba, yale unayoyasema,
Hata mbele kuwe mwamba, ambao umesimama,
Kwa kukiri na kuimba, hauwezi kusimama,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

4. Ingawa umepigika, hali waiona noma,
Ya kwamba umeanguka, mbele mrefu mlima,
Kwa mdomo wako funguka, ujitamkie mema,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

5. Masikio husikia, yale sisi tunasema,
Ni Neno hilo sikia, kwenye hari hujakwama,
Mwenyewe kujiambia, wala si kushika tama,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

6. Tumepewa mamlaka, kuumba tunaposema,
Hilo hasa Neno daka, uone wa Mungu wema,
Kinywa ndicho kimeshika, hazinayo ya uzima,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

7. Kinywani mwako yakaa, mauti pia uzima,
Yanene ya kuchakaa, maisha yako wachoma,
Sema yale ya kupaa, tele yatajaa mema,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

8. Changamoto wapitia, kama wataka kukwama,
Kote unaangalia, namba washindwa kusoma,
Fanya kujitabiria, hakuna kitachogoma,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.

9. Jitabirie baraka, huo hasa ni uzima,
Laana usijetaka, sawa moto kujichoma,
Ulipokwama amka, ili uweze simama,
Wewe uliye dhaifu, sema mimi ni hodari.
(Yoeli 3:10, Kumbukumbu la Torati 30:19)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
_MUOC_

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news