NA LUSUNGU HELELA
WATENDAJI katika Taasisi za Umma wamesisitizwa kuwakaimisha nafasi za madaraka watumishi wenye sifa za kushika nafasi hizo ili kuirahisishia kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI kutekeleza hatua zinazofuata kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Hayo, yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Mara katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa umma.

"Tunawavunja moyo watumishi wenye sifa kwa kuwa baadhi ya viongozi wanakaimisha ofisi kwa watumishi wanaowataka wenyewe na kwa mapenzi binafsi na kusahau kuwa nafasi hizo zipo kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia sifa na vigezo,’’amesema Mhe. Kikwete.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi kufanya kazi zao kwa weledi na kuhakikisha wanafuatilia masuala ya watumishi wao ikiwa ni pamoja maslahi, upandishwaji vyeo na stahiki mbalimbali.
Mhe. Kikwete yuko kwenye ziara ya kikazi mkoani Mara yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo na kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili ili kuzitatua.
