Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) lasisitiza uwekezaji maghala ya kisasa nchini

NA GODFREY NNKO

SERIKALI na wadau mbalimbali nchini wameombwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kisasa ili kusaidia uhifadhi salama wa bidhaa na mazao kwa ajili ya masoko ya ndani na nje.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX),Godfrey Malekano katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

TMX ni taasisi ya 11 tangu vikao kazi hivyo vianze ambapo, mashirika, taasisi za umma zinapata nafasi ya kuelezea zilipotoka, zilipo na zinakoelekea kwa ustawi bora wa umma na Taifa.

"Ili masoko ya bidhaa yaweze kushamiri unahitajika ujazo mkubwa wa bidhaa kwa kufanya uzalishaji mkubwa ili kuweza kuyahudumia masoko mbalimbali.

"Hivyo ni wito wetu kwa Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuwekeza zaidi katika maghala ya kisasa ili kuendelea kuwa na uhakika wa bidhaa za uhakika, bora na za kutosha."

Pia, amesema, Soko la Bidhaa Tanzania ni mfumo rasmi unaokutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja na kufanya biashara ya mkataba inayotoa uhakika wa ubora,ujazo na malipo.

"Mchakato wa kuanzisha soko la bidhaa ulianza muda mrefu kidogo, mwaka 2009 wakati wa uzinduzi wa ule Mpango wa Kilimo Kwanza ambapo mazungumzo makubwa yalikuwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao.

"Ikaonekana kwamba zaidi ya kuongeza uzalishaji kuna suala la masoko,Soko la Bidhaa likatajwa kama moja ya jambo muhimu, kazi ikaanga mwaka 2012 kwa kupata baraka za Baraza la Mawaziri mwaka 2014."

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, mradi wa kuanzishwa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ulizinduliwa Novemba 30, 2015 na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.

"Na Sheria ya Masoko ya Bidhaa ilipitishwa na Bunge mwaka 2015 na kanuni za Soko la Bidhaa zilitolewa na Waziri wa Fedha mwaka 2016, mchakato wa kukamilisha sakafu ya biashara ulianza mwaka 2017 na Soko la Biashara Tanzania lilianza rasmi mwaka 2018."

Amesema, soko hilo huwa linatumia mfumo wa kielektroniki kuendesha minada ya masoko huku muundo wa umiliki ukizingatia ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).

"Kama ilivyoelezwa,Soko la Bidhaa linatumia mfumo wa kielektroniki na tunashukuru mfumo huu umetengenezwa na wataalamu wa ndani wa Soko la Bidhaa.

"Lakini pia wataalamu wengine kutoka taasisi za Serikali kama Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), Wizara ya Kilimo, wote wamehusika ili kuwa na mfumo ambao unaakisi mazingira ya Tanzania."

"Mwanzoni ilionekana tununue tu mfumo kutoka nje, lakini baada ya kuwaleta watu wa nje namna ya kufanya mfumo ufiti mazingira ya Tanzania ikawa ngumu.

"Tukaamua wenyewe kutengeneza mfumo ambao unalingana na mazingira yetu muundo wa umiliki wa Soko la Bidhaa unazingatia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) na kwa sasa soko linamilikiwa na Serikali chini ya Msajili wa Hazina."

"Kwa sasa, Soko la Bidhaa Tanzania linamikiwa na Serikali chini ya Msajili wa Hazina na linasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana,"

Pia amesema, bidhaa nyingi zinaenda katika soko la India ambalo ambako huko kuna soko kubwa la korosho, choroko na mengineyo ambapo tangu kuazishwa kwa soko hilo zaidi ya tani 135,000 za bidhaa zimeuzwa.

"Soko la Bidhaa ni mfumo rasmi unaokutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja wanafanya biashara, kunakuwa na mikataba ya bidhaa inayotoa uhakika wa ubora,ujazo na malipo.

"Kwa hiyo soko la bidhaa sio mnunuzi wa mazao, kazi yetu kukutanisha anayeuza na anayenunua ambapo pale kuna kuwa na mikataba na sisi tunachouza ni taarifa.

"Hata kama mtu ana mazao yake kule Nkasi au Sumbawanga akiweka na kuonesha ubora wake ni kiasi gani, uzito wake kiasi gani, kulingana na tulivyokubaliwa utaratibu wa viwango zile taarifa kupitia mfumo wetu anapata mnunuzi."

"Pia inabidi mazao yawe kwenye magahala ambayo yamesajiliwa na Bodi ya Chakula na Maghala.

"Yale mazao yakishafikishwa pale mwendesha ghala anatoa Quality Insurance kama ni grade' A' atatuletea hizo taarifa na sisi tukishapata hizo taarifa tunasambaza kwa wanunuzi wote wa ndani na nje.

"Ambapo tunapanga sasa siku ya kufanya biashara yetu, ambapo wale wanunuzi wa ndani masharti ya kushiriki ni lazima uweke fedha fulani kwa ajili ya kulinda maslahi ya wenzako wafanyabiashara.

"Bila kupata watu ambao hawaweki kitu chochote tunaweza kupata watu ambao wanakuja kuchezea soko, lazima aweke kiasi kulingana na anavyonunua kulinda masilahi ya washiriki.

"Ni vizuri sana kuweka vigezo ili watu wanaochezea soko wasiwe sehemu ya soko, mauzo yetu yanafanyika kielekitroniki mnunuzi akiwa kona yoyote duniani kama anaweza ku-access mfumo wetu anaweza kufanya biashara soko la bidhaa.

"Kwa wanunuzi wa nje lazima awe na benki yake kule nje ijenge mahusiano ya benki iliyoko hapa Tanzania ambayo ile benki iliyoko Tanzania ndio itamgarantee yule kwamba yenyewe itafanya malipo kwa hiyo bidhaa itakayonunuliwa."

"Kwa hiyo changamoto kubwa iliyoko ni ukiangalia upande wa fedha cash-rate utaona kwamba hakuna tabu, lakini changamoto kubwa ipo kwenye quality na quantity kwa sababu wakati mwingine unaweza ukasema grade A ukapeleka ikawa grade B.

"Kwa hiyo rai yetu kubwa ni Serikali na wadau wengine kuendelea kuimarisha sana hii mifumo hasa mfumo wa chakula ghala ikiwemo wa ushirika, lakini pia hata kule chini kabisa wanalima.

"Kwa sababu quality inaanzia kule chini kabisa, na ni risk kubwa sana kufanya biashara na watu wa nje halafu ukapeleka moja kwa moja vitu ambayo havina ubora.

"Lakini tukiweza kuboresha mifumo yetu ikatoa matokeo yanayotarajiwa ni rahisi kufanya biashara katika mataifa mengi.

"Na kama tunavyojua sasa hivi tunatekeleza sera ya soko la pamoja kwa Afrika kwa hiyo imekuwa na umuhimu sana kuwa na viwango ambavyo vinafafana tuweze kuboresha biashara nchi na nchi na nchi ndani ya Afrika.

"Kuna aina kuu mbili za masoko ya bidhaa,kuna masoko ya papo kwa papo haya yanahusisha mauzo na malipo na uzalishaji wa bidhaa papo kwa hapo.

"Hapa unalipa unachukua hapo hapo na masoko haya pia lengo lengo lake lingine ni future and future option kwenye mifumo ya future na future option ni mauzo ya mkataba unaotekelezwa baadaye.

"Kwa mfano kwa sasa tuko mwezi wa tisa, labda bei ya mahindi kufika mwezi wa Desemba wewe kama mkulima unahisi bei itashuka kwa hiyo unapenda kujihakikishia kiwango cha pesa utakachopata mwezi huo.

"Kwa hiyo wakulima kupitia future contract unaweza ukanunua hiyo contract kwa soko la bidhaa kama la kwetu na ile contract itakupa wewe haki ya kuuza bei ambayo mtakubaliana mwezi Desemba,"amefafanua Afisa Mtendaji Mkuu huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news