MWANZA-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetajwa kuwa nchi ya mfano kwa kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi kwa kuzingatia miongozo ya Kimataifa.
Hayo yamesemwa Septemba 25, 2023 jijini Mwanza na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mhe. Anne Semamba Makinda wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapokea wageni kutoka nchi mbalimbali wanaokuja kujifunza jinsi ya kufanikisha Sensa yenye viwango vya Kimataifa kama tulivyofanya mwaka 2022″, amesisitiza Mhe. Makinda.
Alifafanua kuwa, Mataifa mengi yakiwemo Nigeria na Uganda yamekuja kujifunza NBS namna ya kuandaa Sensa.
Aidha, kutokana na Utendaji mzuri wa NBS unaozingatia miongozo ya Kimataifa, Mhe. Makinda amesema, Tanzania imetajwa kuwa nchi ya pili Afrika katika kuzalisha takwimu zenye ubora baada ya Afrika Kusini ambayo ni ya kwanza Afrika.
Benki ya Dunia iliitaja Tanzania kupitia NBS kuwa nchi inayoshika nafasi ya pili Afrika katika kutoa takwimu zenye ubora.
Kwa upande wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari Mhe. Makinda amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha na kujenga uwezo katika kuwafikishia wananchi matokeo hayo kwa ufasaha ili wayatumie kujiletea maendeleo.
Aliongeza kuwa, Vyombo vya Habari hapa nchini ni wadau muhimu katika usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, vilifanya kazi kubwa ya kuwaelimisha kabla ya Sensa na jukumu hilo lilifanikiwa, kwa sasa tunaomba muendelee ili matokeo ya Sensa yalete maendeleo ya haraka.
Mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara yameandaliwa mahsusi kwa lengo la kuimarisha uwezo wa waandishi katika Kusambaza matokeo ya Sensa kwa kutumia habari wanazotoa katika vyombo vyao vya habari.