TBA mnafanya kazi nzuri-Waziri Bashungwa

DAR ES SALAAM-Waziri wa Ujenzi, Mhe.Innocent Bashungwa ametembelea Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya katika kutekeleza miradi ya Serikali hususani, ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma.

"TBA mnafanya kazi nzuri, tumeona katika ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Wajenzi walikuwa Suma JKT, na TBA mlikuwa Wataalamu na Washauri katika Mradi huo ambao umetekelezwa kwa ubora mkubwa,"anafafanua Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa ametoa rai kwa wapangaji wote waliopanga nyumba za TBA, kulipa madeni yao yote ya Kodi wanazodaiwa ili TBA iweze kutekeleza miradi mingine.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kondoro, ametaja kuwa TBA imekuwa ikidai kiasi cha fedha zaidi ya shilingi Bilioni 81 kwa washitiri mbalimbali na wapangaji wa nyumba hali inayokwamisha utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake.

Amebainisha kuwa TBA, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ushauri na ujenzi kwa ubora.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za makazi kwa watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma, mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi jijini Dodoma, nyumba za majaji katika mikoa minne.

Miradi mingine inatekelezwa katika eneo la Temeke Kota, Magomeni Kota na Masaki jijini Dar es Salaam pamoja na Ghana Kota jijini Mwanza ambapo ujenzi wake unaendelea vizuri.

Ziara ya Waziri Bashungwa kutembelea TBA imelenga kujitambulisha, kujua shughuli zinazotekelezwa, mafanikio pamoja na dira ya mwelekeo katika utekelezaji wa kazi zake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news