Thamani ya Soko la Nyumba yapanda kwa asilimia 6 mwezi Juni 2023

DAR ES SALAAM-Thamani ya soko la nyumba za makazi nchini Tanzania ilikua kwa asilimia 6 katika robo ya pili ya mwaka iliyoishia Juni 30, 2023 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.6 katika robo ya kwanza ya mwaka huu iliyoishia Machi 31, 2023.

Soko lilionesha ukuaji wa asilimia 15 kwa mwaka kutoka shilingi bilioni 509.99 katika robo ya pili ya mwaka 2022 ikilinganishwa na shilingi bilioni 584.59 katika robo ya pili ya mwaka 2023.

Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kampuni ya Kutoa Mikopo ya Nyumba kwa Wakopeshaji Tanzania (TMRC) inaonesha kuwa, katika robo ya pili ya mwaka huu hakukuwa na mtoaji mikopo ya nyumba mpya katika soko.

Idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba ilisilimia 31 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023.

Hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, mikopo ya nyumba iliongezeka hadi shilingi bilioni 584.59, sawa na dola za Marekani milioni 249.92 ikilinganishwa na shilingi bilioni 551.76 sawa na dola milioni 237.53 iliyoripotiwa Machi 31,2023.

Kiwango cha wastani wa mkopo hadi Juni 30,2023 kilikuwa shilingi milioni 102.13, sawa na dola 43,662, ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi milioni 98.60 sawa na dola 42,446 katika robo ya mwaka iliyotangulia.

Aidha, uwiano wa mikopo ambayo haijalipwa ni asilimia 0.33 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 0.3 ya mikopo hiyo katika robo ya mwaka iliyopita.

Katika kipindi hicho cha robo ya pili ya mwaka, wakopeshaji wakuu watano walitoa asilimia 66 ya mikopo yote ya nyumba.

Benki ya CRDB inaongoza kwa kutoa mikopo ya nyumba katika soko nchini ikitoa asilimia 34.15 ya mikopo yote, ikifuatiwa na KCB Bank asilimia 10.5), Azania Bank (7.78), NMB Bank Plc. (7.76) na Stanbic Bank (6.19).

Riba halisi za mikopo ya nyumba iliyotolewa na wakopeshaji ilikuwa wastani wa kati ya asilimia 15 na 19.

Kielelezo-Nafasi katika Soko la Mikopo ya Nyumba-Wakopeshaji Wakuu Watano.

Ukuaji wa haraka wa sekta ya nyumba nchini unatokana na mwendelezo wa ukuaji mkubwa wa uchumi huku ukuaji wa pato la taifa likikua kwa wastani wa kati ya asilimia 6 na 7 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watu, ambapo inakadiriwa kwamba hadi kufikia mwaka 2050 itakuwa mara mbili ya idadi ya sasa; pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na Serikali na taasisi za kimataifa ili kukidhi mahitaji ya nyumba za kuishi za bei nafuu.

Mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi imeendelea kuwa na ukuaji mkubwa kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na sera wezeshi za fedha na bajeti.

Katika kipindi cha mwaka unaoishia Mei 2023, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 22.5 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia ambapo ukuaji wa mikopo ulikuwa asilimia 15.

Mikopo iliyotolewa kwa shughuli binafsi, hasa biashara ndogo na za kati, imeendelea kuchangia sehemu kubwa ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, ikifuatiwa na biashara, uzalishaji na shughuli za kilimo. Mikopo binafsi imechukua sehemu kubwa ya jumla ya mikopo ikifuatiwa na biashara.

Kati ya mikopo hiyo, iliyokwenda kwenye shughuli za kilimo ni asilimia 40.9 na usafirishaji na mawasiliano asilimia 26.7.

Mahitaji ya nyumba kwa Tanzania kwa mwaka yanakadiriwa kuwa ni nyumba 200,000 huku kukiwa na upungufu wa nyumba milioni 3. Kati ya mwaka 2009 na Juni 2023, idadi ya taasisi zinazotoa mikopo ya nyumba imeongezeka kutoka 3 hadi 31.

Jitihada za kuongeza miradi ya nyumba zinaendelea, huko kipaumbele kikubwa kikiwa ni kuendeleza mji mkuu wa Dodoma kufuatia Serikali kuhamishia shughuli za kiutawala.

Riba kubwa na upungufu wa nyumba nafuu ni changamoto zinaathiri ukuaji wa soko la mikopo ya nyumba nchini.

Kampuni ya Kutoa Mikopo ya Nyumba kwa Wakopeshaji Tanzania (TMRC) inaendelea na jukumu lake la msingi la kutoa mikopo kwa wakopeshaji ambazo ndizo zinawakopesha wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news