Uchunguzi, tiba ya mishipa ya damu vyaimarishwa Muhimbili

DAR ES SALAAM-Katika kuboresha huduma za kibingwa nchini Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa kifaa maalum chenye mfumo halisi wa mwili wa binadamu (Simulator).

Ni kifaa ambacho kitatumika kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Tiba Radiolojia (Interventional Radiology) kufanya uchunguzi na matibabu mbalimbali kabla ya kumgusa mgonjwa halisi ambapo katika Ukanda wa Afrika Mashariki kifaa cha aina hiyo kinapatikana Tanzania.

Kifaa hicho kina mifumo yote ya mwili wa binadamu na hivyo kuwawezesha wataalam kujenga uwezo wa kutoa Tiba Radiologia katika mifumo mbalimbali ya mwili.

Kifaa hicho chenye thamani ya shilingi milioni 125 kimetolewa na Kampuni ya Surgical Sciences ya nchini Sweden.

Pia, kampuni hiyo itatoa mafunzo kwa wataalamu wazalendo kuhusu namna ya kuzibua damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu na sehemu mbalimbali za mwili kupitia wataalamu wa Tiba Radiologia wanaotibu mishipa ya damu (ya ubongo) wa Hospitali ya John Hopkins ya nchini Marekani.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa, kwa kuanzia kifaa hicho kitawanufaisha wataalamu wa Tiba Radiolojia ambao watajengewa uwezo wa namna ya kutibu mgonjwa aliyepata kiharusi kwa kuzibua mishipa ya damu katika ubongo kwa kutumia mtambo wa Angio-Suite ili kuwa na ujuzi zaidi katika matibabu hayo.

“Tumepata msaada wa Simulator, lakini wakati huo huo tumepata wataalam wa kutibu mishipa ya damu ya ubongo na sehemu mbalimbali za mwili.

"Kwa hiyo wataalamu wetu wa Radiolojia watapatiwa mafunzo kuhusu namna ya kuzibua mishipa ya damu kwa vitendo kupitia “simulator” wakishafuzu ndio wataweza kuwagusa wagonjwa moja kwa moja,” amesema Prof. Janabi.

Akizungungumza wakati wa kukabidhi kifaa hicho mwakilishi wa Kampuni ya Surgical Sciences, Bw. Anders Melander amesema kuwa, lengo la kutoa msaada huo ni kuimarisha Tiba Radiolojia ambayo inafanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news