UKEREWE NDIKO KWETU: Kajionee mwenyewe,Vivutio vya Utalii vya kila aina

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutangaza vivutio vya utalii nchini ikiwemo vivutio vilivyopo Kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza kama Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza maarufu kama Nyaburebeka.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula (Mb) ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Joseph Mkundi aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa.

Nyaburebeka ni jina la jiwe kubwa linalopatika Kisiwa cha Ukerewe ndani ya Tarafa ya Ukara,mkoani Mwanza ambapo kitu cha kushangaza au kuvutia ni kuwa jiwe hili linacheza.

Kwa mujibu wa chapisho la BBC mwaka 2017, jiwe hilo huanza kucheza mara baada ya mtaalamu wa kulichezesha jiwe hilo kuanza kuliimbia na kuligusa kwa mkono au kulisukuma na mguu mmoja.

Jiwe hili ambalo wataalamu wa kisayansi wanalikadiria kuwa na uzito zaidi ya tani 20,ni uzito ambao kwa nguvu ya mguu wa binadamu wa kawaida hauwezi kulisukuma.

Mwandishi wa BBC,Esther Namuhisa alitembelea eneo hilo na kuweza kuzungumza na mzee Kakuru Makorokoro ambaye ni kiongozi wa familia au ukoo ambao unamiliki jiwe linalocheza.Mzee huyo alibainisha kuwa, jiwe hilo limekuwepo katika Kisiwa cha Ukara kwa karne na karne, likiwa linamilikiwa na ukoo wa familia ya Makorokoro,na kucheza kwake ikiwa ni ishara ya kuenzi mila na tamaduni zao ambazo zimekuwepo kuanzia enzi na enzi za mababu zao hivyo wao pia wamerithi kutoka kwa vizazi vilivyopita vya ukoo wao.(Picha na BBC).

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, jitihada zinazofanywa na Serikali za kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini ni moja wapo ya hatua mahususi ya kufungua fursa za ajira na kustawisha uchumi. Endelea:

1.Ukerewe ndiko kwetu, kumetajwatajwa leo,
Kisiwa cha nchi yetu, kizidi maendeleo,
Kwa kuwavutia watu, vivutio kichocheo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

2.Wizara Maliasili, na Utalii ni leo,
Wameliongea hili, twasubiri matokeo,
Tuwaone watu kweli, wadogo na wenye vyeo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

3.Fukwe kule Ukerewe, ni kama upendeleo,
Kuna mchanga na mawe, kwa matumizi ya leo,
Kajionee mwenyewe, mipango uanze leo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

4.Samaki sijawasema, wafaa kwa kitoweo,
Tena samaki mzima, avuliwa leoleo,
Takula chakula chema, wende ushike koleo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

5.Mapango ya Handebezya, ninayasikia leo,
Sikia Anko Ngerezya, unipe upendeleo,
Nikafike Handebezya, nikufahamu upeo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

6.Kuna jiwe linacheza, natamani nende leo,
Nani analikoleza, liwe kama kipepeo?
Au macho yanacheza, kaone upande cheo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

7.Tambua kama kisiwa, maji huko mchekeo,
Yafaa kuogelewa, kayaone matokeo,
Mazoezi waelewa, kwa afya maendeleo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

8.Hili bado sijasema, jambo la maendeleo,
Kulitoa ni lazima, nisijepigwa fyekeo,
Ukerewe huko kwema, kunao upendeleo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

9.Kama wataka kuoa, nenda ukaoe leo,
Binti za huko ni poa, watu wa maendeleo,
Uliza waliooa, usifwate mapokeo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

10.Watu huko Ukerewe, wengi watu wa kileo,
Nenda ukawaelewe, na ya maendeleo,
Wakwelima tuelewe, tumeshafika upeo,
Kisiwa cha Ukerewe, kwafaa kwa utalii.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news