"Mpaka sasa tunaendelea na tutatembelea viwanja vyote vya ndege. Tumeanza na Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam,kutokana na uwanja ule unatumiwa na wageni wengi zaidi na ndege zinashuka kwa wingi.
"Na mara nyingi hawa wasafirishaji wa dawa za kulevya ni watu ambao wana mbinu mbalimbali za kusafirisha, kuna wakati mwingine zile dawa wanaweza wakazifanya unaona ni kama karanga.
"Kwa hiyo mtu ambaye anakaa kwenye scanner pale, anapoona zile images, kwa sababu kunakuwa na zile image analyisis anaweza kuona ni karanga.
"Kumbe ni dawa za kulevya, namna wanavyozipaki, namna walivyozifunga, kwa hiyo sisi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kutokana na operesheni mbalimbali tunazozifanya na dawa tunazozikamata.
"Kwa hiyo tunapogundua mbinu mpya zinazotumika na unakuta zinafanikiwa kupita,Airport pale, pamoja na kwamba kunakuwa na vile vifaa kutokana na namna alivyofunga zile dawa.
"Kwa hiyo mtu akiona anaweza asibaini kwamba ni dawa, kwa hiyo sisi tunapopata zile taarifa na tunapozibaini zile mbinu tunakwenda sasa kwenye vile viwanja vya ndege.
"Lengo ni kuwafundisha wale ambao wanaokaa kwenye zile scaners ili waone sasa kwamba, dawa za kulevya zinaweza kuja kwa namna tofauti, kwenye images kwa sababu unakuta wanafundishwa kwamba, image hii ukiona rangi hii jua ni dawa za kulevya.
"Sasa na wale wasafirishaji wanabaini hilo, kwa hiyo wanabadili mbinu, kwa hiyo wanabadilisha zile images, kwa hiyo inapoonekana pale inakuwa ni kitu kingine tofauti.
"Kwa hiyo, yeye ameshakariri image yake ni hii, kwa hiyo wale wanapofunga zikiwa tofauti sisi tunapobaini sasa, tunaenda tunawapa elimu.
"Kwa hiyo elimu yetu tunayoitoa ni endelevu, kwa sababu na wao ni wajanja wanabadilisha mbinu, na sisi pia tunapozibaini tunaendelea kuwafundisha wale wafanyakazi wa Serikali walioko kwenye viwanja vya ndege.
"Ni ili waendane sasa na zile mbinu ambazo wanazitumia, tuendelee kuwakamata na tuendelee kuhakikisha kwamba, dawa za kulevya haziendelei kuingia nchini."
Mikakati
"Ukiachana na huo wa kudhibiti usambazaji wa dawa za kulevya, lakini mkakati mwingine ni kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya nchini.
"Demand reduction, kwenye huo mkakati, tunachokifanya tunatoa elimu zaidi kwa wananchi, kwa sababu tumebaini wananchi wengi, hasa vijana wanaingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya bila kujua madhara yake.
"Kwa hiyo, sasa tunachokifanya ni kutoa elimu katika maeneo mbalimbali, shuleni, vyuoni, lakini pia na mitaani ili kuhakikisha kwamba hawaingii.
"Tunapunguza kundi kubwa la watu wanaojiingiza kwenye dawa za kulevya, na ndiyo maana sasa hivyo umeona tumesaini mkataba, MoU na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).
"Ule mkataba tuliosaini ni kwa ajili ya kupanua wigo, wa kutoa elimu kwa sababu kundi kubwa linaloingia kwenye dawa za kulevya ni vijana,hasa walioko shuleni, kuanzia shule za msingi, shule za sekondari na vyuo.
"Na wanatumia zaidi dawa za kulevya,kutokana na lile kundi rika ambalo wanakutana nalo,sasa ukikutana na yule ambaye alishawahi kutumia dawa za kulevya, anashawishi na wengine kutumia.
"Lakini, ushawishi ule unaotumika ni kutokana na wanawapa vitu vyepesi vya kuwaaminisha kwamba, ukitumia dawa za kulevya maisha yatakuwa rahisi, ukitumia dawa za kulevya pengine utakuwa na akili, utakuwa na uwezo mkubwa wa kusoma.
"Sasa, akishajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, mwisho wa siku anakuwa mraibu, akishakuwa mraibu yale malengo yake kwamba atasoma kwa muda mrefu, anaweza labda akawa na maisha rahisi asiwe na mawazo, kwa hiyo anajikuta matokeo yake anasababisha jambo jingine baya zaidi.
"Kwa sababu, unapotumia dawa za kulevya, cha kwanza kabisa, kemikali zilizopo kwenye dawa za kulevya aina zote zinakimbilia kwenye ubongo, cha kwanza kabisa kuharibu ni ubongo, uwezo wa kufikiri.
"Uwezo wa kufanya maamuzi, ndicho kinachoharibika, kabla ya afya, kwa hiyo afya ya akili ndiyo inaathirika ya kwanza halafu yanafuata mambo mengine.
"Na ndiyo maana unakuta wale ambao wanatumia heroin, unakuta wakati mwingine hata nguvu za kutembea, nguvu za kusimama, ule urijali unakuwa haupo, kwa hiyo unakuta hata uwezo wa kufanya kazi unakuwa haupo.
"Na wale wanafunzi ambao wanaingia sasa kwenye dawa za kulevya, mwisho wa siku unakuta hawana tena uwezo wa kusoma, kwa sababu tayari ubongo wake umeshavurugika.
"Kwa hiyo, mwisho wa siku unakuta tunapoteza nguvu kazi,ya wasomi, ya vijana ambao wao ndiyo wanatakiwa kuwa warithi wa kuliongoza hili Taifa.
"Kuendelea kulinda Taifa hili, na kuendelea kuendeleza uchumi wa Taifa hili, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita malengo yake ni kufanya uchumi endelevu.
"Sasa, hauwezi kufanya uchumi endelevu wakati hapa katikati kuna chain inakatika, wale ambao walipaswa kufanya uchumi endelevu wanaishia katikati hapa, hawafiki kwenda kwenye ule uchumi endelevu.
"Na, ndiyo maana sisi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, tumeingia sasa mkataba na TAKUKURU ili kuhakikisha kwamba, hili kundi kubwa tunaliokoa, lisiingie kwenye dawa za kulevya.
"Na unakuta wengi wanaoingia kwenye dawa za kulevya,wengi wana akili sana, kwa mfano operesheni tulizozifanya Dar es Salaam, wengi tuliowakamata, wanafunzi wale wa vyuo unakuta kwamba wana uwezo mzuri wa akili.
"Ukiangalia hata perfomance yao ya darasani ni nzuri,lakini unajikuta ukimuuliza sasa, kwa nini uliingia kwenye dawa za kulevya anakuambia kwamba, niliambiwa nitasoma kwa muda mrefu, pengine nitakuwa na akili nikivuta bangi."
Hali ilivyo
Akizungumzia kuhusiana na tatizo la dawa za kulevya nchini lilivyo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema, "hali kwa sasa ni nzuri, kutokana na operesheni mbalimbali ambazo tumefanya.
"Lakini pia kutokana na mikakati mbalimbali ambayo inafanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
"Ili kuhakikisha dawa za kulevya nchini, zinaisha ipo mikakati mbalimbali ambayo tunaendelea kuifanya. Mkakati wa kwanza kabisa ni kuhakikisha, usambaaji wa dawa za kulevya nchini unaisha kabisa.
"Na ndiyo maana tunaendelea kufanya operesheni mbalimbali, tunaendelea kufanya juhudi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sasa, dawa za kulevya nchini zinaisha, ambayo inaitwa supply reduction.
"Kwa hiyo, hili tunatumia nguvu kubwa, na ndiyo maana unaona pia kwenye mikoa mbalimbali tumekuwa tukifanya operesheni mbalimbali, tunaenda mashambani, milimani, vijijini kumaliza tatizo la dawa za kulevya nchini.
"Na, hizo operesheni tumezianza na tunazifanya nchi nzima, tumeanza na Arusha, tumeingia Kilimanjaro, Morogoro umesikia juzi tulikuwa Iringa, lakini pia Jiji la Dar es Salaam na Pwani, na lenyewe tumeshaligusa.
"Na sasa hivi tunaendelea katika mikoa mingine, lengo ni kuhakikisha kwamba dawa za kulevya, usambaaji wa dawa za kulevya nchini unaisha na hata niko Mwanza ni lengo hilo hilo la kuhakikisha dawa za kulevya nchini linaisha, kwa sababu dawa za kulevya zinaingia kwa njia tatu,"amefafanua kwa kina Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
DCEA nini?
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.
Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995.
Ni ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.