ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewaasa Watanzania waliokabidhiwa vyeti kwa Tajnisi kuendeleza utiifu wa sheria na kuendelea kuishi kwa kujiepusha na vitendo viovu ili wasipotoshe dhamira njema ya Serikali ya kupewa uraia wa Tanzania.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa nasaha hizo Septemba 5, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipowakabidhi vyeti kwa tajinisi Watanzania 3319, wahamiaji wasiohamishika baada ya kukidhi vigezo na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa raia halali nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amewataka Watanzania hao kuipa heshima inayostahili hadhi waliyopewana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa raia, kwa kuwa raia wema.
“Kwa hakika ndugu zangu mna wajibu kwa pamoja tushirikiane kulinda na kudumisha amani tuliyonayo kwa faida yetu, tuliopo sasa na wale watakaokuja baadae,”aliwaasa Watanzania hao.
Rais Dkt.Mwinyi aliwahakikishia Watanzania hao kuwa na haki zote baada ya kuthibitishwa uraia wao kama wanazostahili raia wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, aliwaasa kuzitumia vyema haki na fursa hizo kwa kushiriki kikamilifu kwenye harakati za maendeleo kwa ustawi wa familia zao na Taifa kwa jumla na kuwataka ambao hawajajisajili kufanya hivyo kwa mamlaka husika.
“Natumia nafasi hii kutoa wito kwa ndugu zetu ambao kwa namna moja au nyingine hawajafika kwenye Ofisi za Uhamiaji kujiorodhesha, ni vyema wakaitumia fursa hiyo ili watambuliwe rasmi, Serikali zetu zimedhamiria kulimaliza tatizo hili kutokana na athari zake,”Rais Dkt.Mwinyi aliwasihi.
Sambamba na kuzitaka mamlaka za Serikali na binafsi kuwapa ushirikiano Watanzania hao kwenye masuala mbalimbali kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo kama wanavyofanyia Watanzania wengine.
Katika hatua nyengine Rais Dkt.Mwinyi alitoa wito kwa Idara ya Uhamiaji, kuendelea kuziimarisha sheria zilizopo hususani Sheria ya Uraia wa Tanzania kwa kuifanyia mapitio kwa madhumuni ya kuiwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowahusu wananchi na wageni wanaofika nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni Yussuf akizungumza kwenye hafla hiyo alizipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa busara zao za kuwasamehe Watanzania hao kiasi cha shilingi milioni mbili kama kima cha kulipia uraia wao pamoja na kupongeza ushirikiano kwa Serikali mbili hizo kulifanikisha jambo hilo.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kukamilisha ahadi ya kuzitatua changamoto za Watanzania hao wahamiaji wasiohamishika tangu alipowaahidi mwaka 2020 kuitekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kushughulikia changamoto za Watanzania hao.
Kwa upande wake, Kamisha Jenerali wa Uhamiaji Tanzania, Dkt. Anna Makakala alisema jeshi hilo lina jukumu la kuratibu masuala yote ya uhamiaji nchini yanayohusu raia wanaoomba uraia kisha kukabidhi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Aidha, alieleza Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya zoezi la utambuzi kwa Watanzania hao mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Watanzania hao walikuwa wakikabiliwa na changamoto za kukosa haki zao za msingi kisheria zikiwemo hati za uraia, hati za kusafirikia na haki nyingine wanazopatiwa Watanzania halisi.
Jumla ya Watanzania 3319 wenye asili ya mataifa mbalimbali waliokua wahamiaji wasiohamishika wametambuliwa rasmi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa raia halali wa Tanzania.
Miongoni mwao 3116 wana asili ya Msumbiji, 147 wana asili ya visiwa vya Comorao, watano kutoka Burundi na raia mmoja kutoka Jamhuri ya Rwanda, aidha watoto 1675 pia walitambukliwa.