WAWEZA MBEBA MTU

NA LWAGA MWAMBANDE

AGOSTI 17, 1977 huko Les Ulis nchini Ufaransa alizaliwa mtoto mdogo kwa jina la Thierry Daniel Henry. Baada ya makuzi mema kupitia wazazi wake, baadaye alikuja kuwa mmoja wa nyota wakubwa katika soka la Ulaya na Duniani kwa ujumla.

Thierry Henry ndiye ambaye alikuja kuchukuliwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora wa wakati wote, na mmoja wa wachezaji bora katika historia ya Premier League, pia kuna watu ambao wanamthamini zaidi kwa kuweza kuwabeba katika maisha yao.

Baada ya kustaafu soka tangu mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 37, aliendelea kuwa mkufunzi wa mpira wa miguu wa Ufaransa, mchambuzi na meneja wa timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 21.

Nyota huyo wa Arsenal na mfungaji bora wa timu ya taifa ya Ufaransa aliamua kustaafu baada ya kushiriki soka kwa kipindi cha miaka 20.

Thierry Henry alianza kupata sifa akichezea klabu ya Arsenal katika miaka ya 2000. Mchezaji huyu aliingiza mabao 228 katika mechi 377 tangu alipoanza kucheza hadi siku alipotangaza kustaafu.

Mbali na kuchaguliwa kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry alichezea Arsenal kwa kipindi kirefu, alivaa namba 14 mgongoni kwa kipindi cha miaka minane.

Ni baada ya miaka mingi akipata mafunzo katika klabu ya Monaco, ambapo mechi yake ya kwanza katika klabu ya Monaco aliicheza mwaka 1994.

Thierry Henry alikuwa ni mfungaji bora anayeongoza nafasi ya pili katika Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA), na mchezaji bora nchini Ufaransa mwaka 1997.

Vile vile, Thierry Henry aliichezea pia klabu ya Juventus kwa kipindi cha miezi saba na kupelekea ushindi wa klabu hiyo wa Kombe la Intertoto.

Mfaransa huyo mwaka 1994 alijiunga na klabu ya Monaco akiwa na umri wa miaka 17 ambapo,mwaka 1998 hakucheza wakati Ufaransa ilipotwaa Kombe la Dunia.

Nyota huyo, mwaka 1999 alijiunga na klabu ya Juventus na kuichezea mara 20 ambapo mwaka 1999 alijiunga na Arsenal na kuisaidia klabu hiyo kushinda mataji mawili ya klabu bingwa nchini Uingereza na mataji matatu ya Kombe la FA.

Mwaka 2000 aliifungia Ufaransa mabao matatu na kuisaidia kunyakua taji la Euro ambapo mwaka 2007 alijiunga na Barcelona kwa kima cha Paundi milioni 16.1 na mwaka 2009 aliisaidia Barcelona kushinda ligi na klabu bingwa barani Ulaya.

Hata hivyo, mwaka 2010 alijiunga na New York Red Bulls kabla ya mwaka 2012 kurejea Arsenal kwa mkopo na kufunga mara mbili.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, licha ya umaarufu na utajiri aliokuwa nao Thierry Henry wakati fulani alionesha utu wa namna yake kwa wengine, hivyo kugeuka mbeba majawabu ya ndoto za wengine, unajitolea kusaidia wengine?. Endelea;


1.Kumbe hata wewe hapo, waweza mbeba mtu,
Ni huyo mwandishi hapo, na Thierry mwenye utu,
Kumpata papo hapo, maisha yakawa kwatu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

2.Huyu Karim Bennani, anatufundisha kitu,
Kijitolea kazini, akiwa mwanafunzi tu,
Likabidhiwa mpini, ampate Thierry tu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

3.Kwamba angefanikiwa, kumpata huyo mtu,
Angeweza ajiriwa, maishani awe mtu,
Wala hakutegemewa, atafanya hicho kitu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

4.Karim akajaliwa, kumpata huyo mtu,
Ujasiri lijaliwa, bila ya kujali kitu,
Kasema ya kuelewa, kumwingia yule mtu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine.

5.Thierry Henry yule, maarufu yule mtu,
Uwanjani enzi zile, alifanya vingi vitu,
Hasa Arsenali kule, libeba vingi viatu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

6.Kwa umaarufu wake, kumsikiliza mtu,
Atumie muda wake, asiyemjua mtu,
Alifanya utu wake, kumbe amjenga mtu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

7.Pale alipokubali, kwa ombi la yule mtu,
Kuwa tayari kwa kweli, mahojiano kiutu,
Kwake ajira kamili, sababu ya huyu mtu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

8.Henry angekataa, vile hamjui mtu,
Kijana angechakaa, kazi asipate kitu,
Ngebaki ang’aang’aa, mtu asiye na kitu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

9.Watu walofanikiwa, jitahidi fanya kitu,
Wale wasofanikiwa, wapate kuwa ni watu,
Kutoa wabarikiwa, hata kwa kidogo kitu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

10.Somo la kijana huyu, kwake faida na kwetu,
Thierry Henry huyu, pia ni elimu kwetu,
Ni kweli siyo ubuyu, amefanikiwa mtu,
Vipi unajitolea, kusaidia wengine?

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news