DAR ES SALAAM-Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), amekabidhi ofisi rasmi pamoja na Vitendea kazi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Yusuph Makamba (Mb) aliyeteuliwa kuwa Waziri mwenye dhamana ya kuiongoza Wizara hiyo.
Makabidhiano ya viongozi hao yamefanyika leo tarehe 09 Septemba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salam.
Uhamisho na uteuzi huo unafuatia Mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 30 Agosti, 2023 na kuwaapisha Mawaziri na makatibu wakuu aliowateua tarehe 01 Septemba, 2023, alipomhamisha Dkt. Stergomena kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na nafasi yake kuchukuliwa na Mheshimiwa January Makamba aliyekuwa Waziri wa Nishati.
Akiongea na Menejimenti ya Wizara mara tu baada ya kumalizika kwa shughuli ya kukabidhiana ofisi, Mheshimiwa Dkt. Stergomena ameishukuru Menejimenti pamoja na watumishi wote kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi chote cha miezi kumi na moja alichokuwa Waziri wa Wizara hiyo.
Aidha, Dkt. Stergomena amemweleza Mheshimiwa Makamba kuwa anamkabidhi kijiti alichokipokea kutoka kwa mtangulizi wake Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula.
Mabadiliko aliyoyafanya Mheshimiwa Rais yanalenga kuboresha utendaji serikalini. Ni matarajio yake kuwa Mheshimiwa Makamba atamsaidia vyema Mheshimiwa Rais kujenga Diplomasia ya uchumi, ili maono yake yaweze kutimia. Vile vile amemuahidi kila aina ya ushirikiano atakaouhitaji.
Kwa upande wake Mheshimiwa Makamba amemshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Stergomena kwa kuwa amekuwa msaada mkubwa kwake na mashauri mwema katika kutekeleza majukumu yake.
Aidha, ameahidi kuyaendeleza mazuri yote aliyoyaacha. pia, amempongeza kwa kuendelea kuaminiwa na kuteuliwa na mwisho akamtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye Wizara aliyowahi kuiongoza (Wizara ya Ulinzi na JKT).
Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Mawaziri wa Wizara hiyo ambao ni Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) ) anayesghulikia masuala ya Mambo ya Nje na Mheshimiwa Stephen Byabato (Mb) anayesghulikia masuala ya Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu Balozi Shelukindo (Mammbo ya Nje) na Katibu Mkuu Mteule Bw. Stephen Mbundi (Afrika Mashariki) pamoja na Wajumbe wa Menejimenti.