Waziri Kairuki:Tangazeni vivutio vya utalii nchini

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amevitaka vyombo vya habari kutangaza vivutio vya utalii ili watalii wengi waweze kuvifahamu na kuja nchini hatimaye kuinua uchumi wa nchi yetu.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo Septemba 25,2023 wakati alipotembelea runinga ya Taifa TBC jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa kituo hicho.

Ni kabla ya kufanya kipindi maalum kwa ajili ya kutoa ujumbe maalum wa Tanzania katika Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ambapo kauli mbiu ya siku hiyo kwa mwaka huu ni Utalii na Uwekezaji Unaojali Mazingira.
Aidha, amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia chaneli yake ya utalii ya “Safari Channel” kufanya tafiti za kuboresha matangazo vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani na kujifunza kwa nchi zenye teknolojia ya juu ya utangazaji wa vivutio hivyo ili iweze kutangaza vivutio vya utalii duniani.

“Ninawataka mtoke mwende duniani mkajifunze wenzetu wanaendeshaje chaneli za utalii ili na sisi tuweze kuendesha kituo chetu vizuri zaidi kiweze kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani na kutuletea wageni wengi zaidi,”amefafanua Mhe.Kairuki.

Amesema, dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa tunatangaza vivutio vya utalii watu wengi waweze kufahamu hazina ya vivutio vya Tanzania tulivyonavyo ili waweze kuja kutembelea na kuliingizia taifa mapato zaidi.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini kusimamia Sekta za Maliasili na Utalii na kumhakikishia kuwa ataendelea kushirikiana na menejimenti ya wizara yake na wadau mbalimbali kutekeleza maono ya Serikali na ya Mhe. Rais kutangaza utalii wa Tanzania.

Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yanafanyika jijini Ryadh nchini Saudi Arabia ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia inashiriki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news