WAZIRI MKUU AKAGUA KITUO CHA AFYA KAKUNYU, ATOA SIKU 5 KIANZE KAZI

*Ahimiza kilimo, mbolea, utunzaji wa mazingira 

KAGERA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa kituo cha afya cha Kakunyu kilichopo km. 75 kutoka tarafa ya Bunazi, wilayani Missenyi na kutoa siku tano kiwe kimeanza kufanya kazi. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua miundombinu katika kituo cha afya cha Kakunyu kilichopo Missenyi, Mkoani Kagera, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa. Kituo hicho kimegharimu shilingi milioni 500, Septemba 23, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa agizo hilo Jumamosi, Septemba 23, 2023 mara bada ya kukagua kituo hicho, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika kijiji cha Bugango, wilayani Missenyi, mkoani Kagera. 

"Mkurugenzi, hawa madaktari wameletwa kufanya kazi. Watafutie meza, dawa zipo, wape makaratasi yao waanze kuhudumia wananchi. Nakupa siku tano, hapo mapokezi na vyumba vya madaktari vianze kazi sababu hawa tayari wapo hapa kijijini," amesema wakati akimpa maelekezo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga. 

Waziri Mkuu alikagua majengo yaliyokamilika ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, wodi ya wazazi na kliniki ya uzazi na mtoto (RCH). Kituo hicho kimegharimu sh. milioni 613 ambapo sh. milioni 523 ni za mapato ya ndani na sh. milioni 90 zilitoka Serikali kuu ambazo zimetumika kujenga nyumba moja ya kuishi watumishi watatu (3 in 1). 
Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba sh. milioni 150 zimekwishatolewa na Serikali ya awamu ya sita ili zitumike kununua vifaa tiba vya kituo chao. Alipoulizwa kuhusu uwepo wa fedha hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Isesanda Kaniki alikiri kuwa fedha hizo zimeshapokelewa na zimetumwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kulipia vifaa tiba hivyo. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakazi hao wachangamkie fursa za kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa sababu kilimo ni fursa, kilimo ni uchumi na kilimo ni maisha. 
“Endeleeni kulima mazao ya miezi mitatu mitatu kama maharage na mahindi, ili muweze kuuza nchi za jirani. Mheshimiwa Rais alitoa sh. bilioni 50 za ruzuku ya pembejeo hasa mbolea ili mpate mbolea hiyo na kuzalisha zaidi mazao. Jiandikisheni ili mpate namba za kudumu za kielektroniki za utambulisho. Namba hizi zitawasaidia kupata unafuu wakati wa kununua pembejeo,” alisema. 

Aidha, aliwataka wakazi hao watunze vyanzo vya maji dhidi ya mifugo na ukataji miti hovyo kwani uharibifu wa vyanzo vya maji ni mkubwa. “Uharibifu ni mkubwa na mifugo mingi ilikuwa inaingia kuja kuharibu vyanzo na sisi wenyewe hatuvilindi. Serikali zote za vijiji na Kamati za Mazingira nenda muwe wakali dhidi ya watu wanaoharibu vyanzo vyetu ili tupate maji mengi kwa ajili ya matumizi ya vijijini, majumbani na mashambani.” 
“Wenyeviti wa vijiji na kamati zenu za maendeleo za kata, simamieni eneo la mazingira kwani hali si nzuri. Duniani leo, kuna mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, hata majira ya mvua yamebadilika. Kwa nini? Ni kwa sababu tumeharibu vyanzo. Nani ameharibu? Ni sisi wenyewe. Nani atavilinda? Ni sisi wenyewe. Hebu tuvilinde vyanzo vyetu,” alisisitiza. 

Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu na leo atazuru wilaya ya Muleba. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news