WAZIRI MKUU AKAGUA SOKO LA KIMATAIFA LA DAGAA

KAGERA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa uendeshaji wa soko la kimataifa la mazao ya uvuvi la Magarini ikiwemo kuajiri mtumishi wa Serikali atakayesimamia makusanyo.

“Lete Afisa Mapato hapa badala ya kutoa ajira kwa vibarua; eneo hili litawasaidia kupata mapato mengi ambayo yatasaidia kuendesha soko hili ikiwemo kuweka taa za barabarani. Wavuvi wenu wahudumiwe na wasaidiwe ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi,” amesema wakati akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi huyo, Dkt. Peter Nyanja.
Ametoa wito huo leo Jumapili, Septemba 24, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Magarini na wafanyabiashara mara baada ya kukagua bandari ya Magarini na Soko la Kimataifa la mazao ya Uvuvi la Katembe - Magarini lililopo kata ya Nyakabango, wilayani Muleba, mkoani Kagera.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kufanya shughuli zao kwa tija. “Rais Dkt. Samia ameweka nguvu ili kuwanufaisha wavuvi ikiwemo kununua boti 1,200 kwa ajili ya vikundi vya wavuvi ili kuwawezesha wavue mbali zaidi.”

Katika mwaka fedha 2022/2023, soko hilo linalohudumiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Halmashauri ya Muleba lilizalisha tani milioni 26.96 za dagaa na samaki kutoka visiwa vya Bumbire, Maziga, Ikuza, Kerebe na Goziba.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuelekeza Meneja Bandari - Kanda ya Ziwa Victoria, Bw. Erasto Lugege afanye maboresho ya bandari ya Magarini kwenye eneo la jengo la abiria na gati.

Vilevile, amezitaka taasisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya HIfadhi za Taifa (TANAPA) na Halmashauri ya Wilaya zikae pamoja na kupanga vizuri eneo hilo ili liwe kivutio.

“Malengo yetu ni kuongeza kituo cha TANAPA ili shughuli za utalii zianzie hapa kwenda kwenye hifadhi ya Rubondo badala ya kuzunguka hadi Chato,” alisema.

Akitoa taarifa yake, Meneja Bandari - Kanda ya Ziwa Victoria, Bw. Erasto Lugege alisema kwenye bajeti ya 2023/2024 wanatarajia kuboresha gati hilo ambalo lilifunikwa na maji tangu mwaka 2020 kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news