Waziri Mkuu asema Rais Dkt.Samia yuko imara,awacharukia watendaji

TANGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wa Handeni na Watanzania kwamba Rais Samia Suluhu Hassan yuko imara na amewahimiza watendaji wa Serikali wajipange kumsaidia ili atimize maono yake.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wake, Septemba 29, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Nataka niwahakikishie kwamba Rais wetu yuko imara sana, yuko imara sana, anafanya kazi yake vizuri ila ni sisi watendaji ndiyo tunamuangusha. Kuanzia sasa hiyo kitu hamna; tutabanana na Halmashauri mjipange,” alisema.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jioni ya Septemba 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, iliyojengwa eneo la Mkata-Mbweni, mkoani Tanga.

Akisisitiza juu ya usimamizi wa miradi ya Serikali, Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi wewe siyo desk officer, wewe ni field officer; simamieni watu wenu. Kama umekuja juzi au mwaka jana au ulikuwepo, nendeni site mkeshe huko na kuhakikisha kazi zinafanyika. Zamani tuliwasema Wakuu wa Idara lakini sasa tunataka Wakurugenzi muwajibike.”

Waziri Mkuu alisema Rais Samia aliingia madarakani mwaka 2021 na kutoa fedha nyingi za miradi mbalimbali lakini cha kushangaza kuna watu hadi leo hawajamalizia ujenzi wa hiyo miradi. “Kuna kasoro kubwa imejitokeza ni watu walipata fedha yote lakini majengo hayajaisha. Yeyote aliyepokea fedha za mwaka 2021 au 2022 na kazi bado haijaisha, ajue kuwa hayuko salama. Si Handeni wala kwingineko, yeyote ambaye hajamaliza ujenzi hatutamvumilia,” alisisitiza.

“Natoa agizo kwa Wakuu wa Wilaya, pitieni kwenye miradi yenu na muangalie ni miradi ipi ilipokea fedha mwaka 2021 na je leo inatumika? Hivi inakuwaje zahanati ya tangu mwaka 2022 hadi leo haijamalizika? Kwani kujenga zahanati inahitaji matofali mangapi, mabati mangapi, na inahitaji kuwa na vyumba vingapi?,” alihoji Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi na watendaji wanaosimamia mradi huo na kuwataka waendelee kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa na wananchi waweze kunufaika na huduma zote muhimu.

“Mkurugenzi wa Halmashauri hakikisha vifaa vilivyonunuliwa na vitakavyonunuliwa, vinatunzwa vema pamoja na majengo yote yaliyopo. Tunzeni pia miundombinu mingine yote iliyopo, kumbukeni mradi huu umegharimu fedha nyingi za kodi za Watanzania pamoja na fedha za wafadhili,” alisema wakati akimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Bw. Saitoti Stephen.

Aliitaka Halmashauri iweke mkakati wa ukarabati wa miundombinu iliyopo ili kuepusha gharama za matengenezo makubwa. Pia akawataka waweke mpango mahsusi wa kutunza mazingira kwa kupanda miti inayokubaliana na hali ya hewa ya mahali hapo.”

Alisisitiza kuwa fedha inayopelekwa kwa ajili ya kutelekeza miradi iwe ya Serikali au ya wafadhili itumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa. “Halmashauri mjipange, kazi iendelee, na iendelee kwa ubora,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news