Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni

TANGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwasisitiza viongozi waisimamie na kuikamilisha mapema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga, Septemba 29, 2023. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba na wa tatu kushoto ni Sheykh Abdallah wa Taasisi ya Alnour Society inayochangia katika ujenzi wa hospitali hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Madiwani wa Halmashauri hii lazima mjione mna bahati sana. Mlianza kwa kutenga sh. milioni 500 lakini akaja mwekezaji kutoka Serikali ya Kuwait na kuunga mkono juhudi zenu na leo mna hospitali kubwa sana. Nimekagua jengo la utawala, kazi ni nzuri,” alisema.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jioni ya Septemba 29, 2023 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mara baada ya kukagua ujenzi huo na kuweka jiwe la msingi kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, iliyojengwa eneo la Mkata-Mbweni, Tanga.

Alisema, anatambua changamoto waliyonayo ya watumishi kwani waliopo ni 47 wakati mahitaji yao ni 247. Alisema ajira zinatoka kisekta na akawaomba waendelee kuwa wavumilivu na kuiamini Serikali yao.

Akielezea kuhusu changamoto ya upatikanaji wa magari ya kubeba wagonjwa, Waziri Mkuu alisema kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaagiza magari ya wagonjwa kwa ajili ya nchi nzima na kwamba yako kwenye taratibu za kuingizwa nchini. “Magari hayo yakifika, hapa Mkata mtapatiwa magari mawili ambapo moja ni la kubebea wagonjwa na jingine ni la Mkuu wa Kituo kwa ajili ya kukagua huduma za afya.”

Akifafanua hoja kuhusu gari la zimamoto, Waziri Mkuu alisema utaratibu wa kununua magari hayo upo chini ya Halmashauri zenyewe na siyo Serikali kuu kwani mnatambua hatari zilizopo na kati ya mipango yenu ni kununua gari la zimamoto ili muweze kuzima pale ambapo kuna dharura, kwa hiyo Halmashauri inapaswa kutenga fedha za kununulia hayo magari. “Ongezeni mapato na simamieni mapato mnayokusanya,” alisema.


Waziri Mkuu aliwashukuru viongozi wa taasisi za Shaykh Abdullah Al-noury Charity Society na Islamic Help pamoja na mwakilishi Balozi wa Kuwait nchini Tanzania kwa msaada wao mkubwa ambao alisema utaokoa maisha ya Watanzania wengi.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo, Mkuu wa Idara ya Afya, Lishe na Kinga, Dkt. Kanansia Shoo alisema Halmashauri hiyo ilipokea sh. bilioni 6.51 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 3.45 zilitoka Serikali Kuu, sh. milioni 57 ni za mapato ya ndani na sh. bilioni 3 ni fedha za mdau wa maendeleo Shaykh Abdullah Al-noury Charity Society chini ya usimamizi wa Taasisi ya Islamic Help.

Dkt. Shoo alisema jumla ya sh. bilioni 2.43 kutoka Serikali kuu, zilijenga majengo nane ambayo ni wodi za wanawake na wanaume, jengo la wagonjwa wa nje kwa awamu ya kwanza, bohari ya dawa, maabara, jengo la upasuaji, la huduma ya dharura (EMD) na wodi ya watoto.

“Mkataba wa makubaliano kati ya Halmashauri na Islamic Help ulisainiwa tarehe 30/04/2021 na kazi ilianza rasmi tarehe 15/08/2021. Mkataba huo wa sh. bilioni 3 ulikuwa ni kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya hospitall. Kati ya hizo, sh. bilioni 2.4 zimetekeleza ujenzi wa majengo sita ambayo ni ukamilishaji wa jengo la OPD lenye ghorofa moja, jengo la wajawazito lenye chumba cha upasuaji, jengo la mionzi, la kufulia, la kuhifadhia maiti, la kichomea taka, njia za wagonjwa (walk ways) na uzio. Sh. milioni 600, zimetumika kununua vifaa vya hospitali na samani,” alisema.

Alisema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD), huduma za dharura, wagonjwa wa kulazwa, kliniki ya baba, mama na mtoto, chanjo, huduma za kujifungua na upasuaji, maabara, ultrasound na huduma za kuhifadhi maiti.

“Kuanzia Juni mosi, 2023 hadi Septemba 27, 2023 jumla ya wagonjwa 2,300 walipata huduma ambapo waliolazwa walikuwa ni 247 na wagonjwa wa nje ni 2,053. Akinamama waliojifungua ni 58 kati ya hao 36 wamejifungua kawaida na 22 wamejifungua kwa upasuaji. Majeruhi wa ajali za barabarani ni 43 kati yao 14 wamepewa rufaa kwenda Muhimbili pamoja na Bombo,” alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news