Waziri wa Fedha awaita wawekezaji kutoka nchi za Scandinavia

NA BENNY MWAIPAJA
Stockholm,Sweden

WAZIRI wa Fedha, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), amewahakikishia wawekezaji katika nchi za Scandinavia ikiwemo Sweden kuwa Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kupitia upya masuala ya kodi na kifedha ili kuvutia uwekezaji zaidi wa mitaji kutoka nje ya Tanzania.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akishiriki Mkutano wa Wawekezaji Mjini Stockholm, Sweden, ikiwa ni mkakati wa Ubalozi wa Sweden nchini humo, ukiongozwa na Balozi Mhe. Grace Olotu, kuzungumza na wawekezaji na kuwaeleza fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

Dkt. Nchemba amesema hayo aliposhiriki mkutano wa wawekezaji, mjini Stockholm, Sweden, ulioitishwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Grace Olotu, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Ubalozi huo kuimarisha masuala ya diplomasia ya kiuchumi.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania ni sehemu ya kimkakati ya kibiashara kutokana na ukubwa wa idadi ya watu waliopo katika eneo lote la Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Ukanda wote wa Maziwa Makuu na kwamba Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuwataka wawekezaji hao wasaidie kuwahamasisha wawekezaji wengine zaidi kutoka nchi hizo za Scandinavia, kuwekeza nchini.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bw. Japhet Justine, wakiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MTI, ambaye amewekeza nchini Tanzania, Dkt. Pontus Engstrom, baada ya kushiriki Mkutano ulioitishwa na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Ubalozi huo kuimarisha masuala ya diplomasia ya kiuchumi kwa kuvutia Mitaji na Teknolojia kutoka katika nchi za Scandinavia. Mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya ECA Marriot, Stockholm, Sweden. 

Alipigia chapuo maeneo muhimu ya uwekezaji yatakayokuza ajira na mauzo nje ya nchi kikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi, maeneo ambayo Serikali imewekeza fedha za kutosha lakini inahitajika mitaji na teknolojia itakayoongeza thamani ya mazao yatakayouzwa nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni. 

Pia alishawishi uongezaji thamani kwenye madini ndani ya nchi ikizingatiwa Tanzania ina madeni muhimu kama Nickel, Lithium na pia Graphite. Fursa kubwa kwenye kuanzisha viwanda vya madawa ya binadamu.
Aidha, aliieleza jumuiya hiyo ya wawekezaji kuwa hali ya uchumi wa Tanzania inaendelea kuimarika licha ya changamoto ya UVIKO 19, Vita baina ya Ukraine na Urusi, pamoja na kuyumba kwa soko la fedha za kigeni.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu, alisema mkutano huo na wawekezaji umelenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na nchi hiyo ulioanza tangu miaka ya 1930, na kwamba mkazo mkubwa hivi sasa ni kuimarisha zaidi diplomasia ya uchumi kwa kushawishi uwekezaji zaidi wa mitaji.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), (wa pili kulia) akisikiliza hoja na ushauri wa wawekezaji, mjini Stockholm, Sweden, wakati alipopewa fursa ya kuzungumza na wawekezaji hao, ikiwa ni jitihada za Balozi wa nchi hiyo, Mhe. Grace Olotu, ambapo walizungumzia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania. Kulia ni Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bw. Japhet Justine, wa Pili kulia ni Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Mhe. Grace Olotu, na Kiongozi wa wawekezaji walioshiriki mkutano huo, ambayepia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MTI, ambaye pia amewekeza nchini Tanzania, Dkt. Pontus Engstrom.

Kwa upande wao, baadhi ya wawekezaji hao ambao wamewekeza mitaji na tenolojia katika miradi mbalimbali wanayoitekeleza Tanzania Bara na Visiwani, wamepongeza hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hatua iliyowafanya wawekezaji wengine wengi kuendelea kutaka kuwekeza nchini Tanzania.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb)(katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Grace Olotu (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MTI Bw. Pontus Engstrom (wa pili kushoto)), Meneja Miradi wa Kampuni ya SWECO Bi. Ana- Karin Municio (kulia), na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bw. Japhet Justine (kushoto), pamoja na baadhi ya wawekezaji walioshiriki mkutano ulioitishwa na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Ubalozi huo ya kuimarisha masuala ya diplomasia ya kiuchumi.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Stockholm, Sweden).

Dkt. Nchemba na ujumbe wake wako katika ziara ya kikazi nchini Sweden, ziara iliyolenga kuimaisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Sweden na Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news