Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na wadau wa huduma za uchunguzi

DODOMA-Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana na wadau wa huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kuimarisha huduma za uchunguzi wa maabara, Vifaa-Tiba, damu salama pamoja na ubora wa huduma ili kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu. 
Hayo ameyasema leo Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi Dkt. Alex Magesa wakati akifungua mkutano wa kitengo cha huduma za uchunguzi wa magonjwa pamoja na wadau wa huduma za uchunguzi wa magonjwa kilichofanyika Jijini Dodoma. 

“Tunaendelea kushirikiana na wadau hawa ili kuondoa kero kwa wananchi ambapo miongoni mwa kero hizo ni pamoja na upatikanaji wa Vitendanishi, Vifaa, Vifaa-Tiba ikiwemo ya mionzi na upande wa damu salama,”amesema Dkt. Magesa.
Amesema, ili kufanikisha hayo lazima kazi ifanyike Kama timu ambapo kikao hicho kikimalizika wajumbe wataondoka na maazimio ambayo yatawezesha kwa kila mmoja kujua majukumu yake na anasaidiaje katika kufikia malengo makuu ya Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla. 

“Lengo la mkutano huo ni kuwasiliana na kujadili vipaumbele vya huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa wadau wote ili kuweka mikakati ya pamoja ya kufikia malengo ya Wizara ya Afya katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa,”amesema Dkt.Magesa.
Aidha, Dkt. Magesa amesema, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alitoa malengo mbalimbali ambayo yanatakiwa kutekelezwa kwa wakati ili kutatua kero za wananchi ndio maana wameamua kuitisha nguvu ya pamoja ikiwemo nguvu za wadau. 

“Katika kutekeleza malengo aliyoyatoa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ndio maana tumeamua kukutana ili tuweze kujadiliana namna ya kutekeleza maelekezo hayo ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa urahisi na haraka,”amesema Dkt. Magesa.
Pia, amesema kwenye mashirikiano hayo yatawezesha kusongesha gurudumu la maendeleo katika upande wa uchunguzi na kutoa huduma zilizo bora ili kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

“Lakini pia mashirikiano haya yatawezesha kupatikana kwa wakati takwimu sahihi ili kuhakikisha tunaleta huduma za uchunguzi wa haraka kwa wananchi na wananchi wafurahiye matunda ya uwekezaji kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia na Waziri wetu Mhe. Ummy Mwalimu (MB),”amesema Dkt. Magesa.
Mwisho, Dkt. Magesa amesema bila uchunguzi Idara ya uchunguzi hakuna huduma za tiba ambazo zitaendelea nchini hivyo mategemeo ni kwamba uchunguzi bora unatoa matibabu bora kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news