Wizara ya Afya yawajengea uwezo wanahabari Dodoma

DODOMA-Wizara ya Afya kupitia Idara ya Tiba imetoa mafunzo ya ugonjwa wa Sikoseli kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma zaidi ya vyombo 40 kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili waweze kupata uelewa na kuweza kusaidia kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo.

Hayo ameyasema leo Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Caroline Damian wakati akifungua semina kwa waandishi wa habari juu ya ugonjwa wa Sikoseli iliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.

“Mwezi wa Tisa ulimwenguni kote tunazimisha mwezi wa uelewa wa Sikoseli kwa jamii, hivyo tumeanza kutoa elimu kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma zaidi ya vyombo 40 ili waweze kusaidia kuielimisha Jamii juu ya ugonjwa huo,”amesema Dkt.Caroline.

Aidha, Dkt. Caroline amesema kuwa mchango wa waandishi wa habari ni mkubwa sana Katika kuwafikia wananchi hivyo wataweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi kwa kuwapa elimu juu ugonjwa huo wa Sikoseli ili kupunguza tatizo hili hapa nchini.

“Tunaamini kwamba waandishi wakielewa vizuri watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujibu maswali na kutoa elimu kwa Jamii ya kutosha,”amesema Dkt.Caroline.

Pia, Dkt. Caroline amesema kuwa kuna dhana potofu nyingi katika jamii kuhusiana na ugonjwa wa Sikoseli kwa sababu ni ugonjwa wa kurithi hivyo waandishi wa habari ni kundi muhimu sana litakaloweza kwenda kutoa elimu kwa jamii waondokane na dhana potofu hiyo.

Hata hivyo, Dkt. Caroline ameiasa Jamii kupata elimu sahihi juu ya ugonjwa huo wa Sikoseli ambapo itawawezesha wasimamia Sera ya Afya kuweza kuwapata Watoto waliopo kwenye Jamii wenye ugonjwa huo ili waweze kupatikana matibabu sahihi.

“Jamii ikipata uelewa vizuri ambao ni sahihi itawezesha kuondokana na dhana potofu ambapo inapelekea wengine kuwaficha watoto wao hivyo itasaidia kupatikana kwa watoto wenye tatizo hilo na kuwapatia tiba sahihi sababu ukiwa na ugonjwa wa Sikoseli unaouwezekano mkubwa wa kupona,"amesema Dkt.Caroline.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news