Wizara ya Elimu yatangaza watafiti 47 walioshinda tuzo

DODOMA-Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetangaza watafiti 47 kutoka taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi, ambao wameshinda tuzo kwa kuchapisha matokeo ya utafiti waliofanya kwenye majarida yenye hadhi ya juu kimataifa katika nyanja za afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati.
Akizungumza Septemba 16,2023 jijini Dodoma katika hafla ya kutangaza washindi hao, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kila chapisho lililofikia vigezo, mhusika atapata Sh50 milioni, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuongeza hamasa na morali kwa watafiti katika maeneo ya sayansi na teknolojia.

“Kila chapisho lililoshinda limetengewa Sh50 milioni. Tunataka wahadhiri wetu wawekeze muda, akili na nguvu katika kufanya tafiti ambazo zitatatua changamoto katika jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa,”amesema Prof. Mkenda na kuongeza:
“Serikali inaona haja ya kuwawezesha wanasayansi wetu katika utafiti; tunachokifanya ni kidogo lakini kinatuma salamu. Tunataka mtafiti aweze kuchuma maisha yake kutokana na utafiti.” 

Amesema fedha walizopata zitachagiza wengine kujikita kwenye utafiti wenye tija kwa Taifa na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
“Tunataka watafiti wajikite kwenye utafiti na si kufanya biashara ili wapate fedha. Tunataka waende kwenye majarida hayo, ili utafiti wao ujiuze kimataifa na kuwezesha kujikwamua kiuchumi,”amesema Prof. Mkenda.

Wakati huohuo, Waziri amezindua awamu ya pili ya uwasilishaji wa machapisho yaliyochapishwa kati ya Julai Mosi 2022 na Mei 31, 2023 katika nyanja za sayansi ya kilimo na mifugo, uhandisi na Tehama. Alitaja tarehe ya mwisho kuwasilisha machapisho hayo ni Oktoba 31, 2023.
“Katika mwaka wa fedha 2022/23, bajeti iliyopitishwa ilikuwa Sh bilioni moja, sasa tumetumia Sh 500 milioni katika nyanja za afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati. Tunafungua tena dirisha ili kuchukua nyanja tulizoacha ambazo machapisho yake yamo ndani ya kipindi hicho ,”amesema.

Amesema kwa wale ambao machapisho yao yalianza kuchapishwa Juni Mosi 2023, dirisha hilo litatangazwa baadaye.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya tathmini ya machapisho hayo, Prof. Yunus Mgaya kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema machapisho 82 yalipokelewa na kamati hiyo kutoka kwa watafiti wa taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi, kwenye maeneo ya afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati.

“Baada ya mchakato kukamilika, machapisho 20 ambayo kati yake 10 ni mkondo wa sayansi asilia na hisabati na 10 kutoka mkondo wa afya ya sayansi tiba, tulibaini yamekidhi vigezo vya kupata tuzo,”amesema.
Alibainisha kuwa ndani ya machapisho hayo kuna Watanzania 47 ambao wamekidhi kupata tuzo hizo zinazogharimu shilingi 500 milioni.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo imesisitiza katika tuzo zijazo, waombaji wahakikishe wanawasilisha wasifu binafsi na barua za uthibitisho kutoka taasisi wanazofanyia kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news