Bangi na mirungi hazikubaliki katika ardhi ya Watanzania-Rais Dkt.Samia

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa wakuu wote wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa,wanawaongoza wananchi ili kuachana na kilimo cha bangi na mirungi, badala yake wajishughulishe na kilimo kingine hususani mazao ya chakula kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa wito huo Oktoba 14, 2024 wakati akizungumzia tatizo la dawa za kulevya nchini katika Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa Wilaya ya Babati mkoani Manyara.  

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa ni "Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa."

"Kwa hiyo niwaombe sana wakuu wote wa mikoa na wilaya kwenda kusimamia masuala haya, pamoja na kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa, na hivi karibuni mmeshuhudia Serikali kupitia idara ile ya kupambana na dawa za kulevya (Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini-DCEA).
"Jitihada zile zimeonesha sana kupambana na dawa zile katika maeneo ya Arusha na Kilimanjaro, sasa nikawa ninajiuliza hivi ndugu zangu wa mikoa hiyo inayootesha hayo mazao, bangi, mirungi na mengineyo hawakuona biashara nyingine yoyote ila biashara hii?.

"Sasa niwaombe sana, twende tukasimamie upandaji wa mazao mengine, na kwamba mazao haya waliyoazoea hayakubaliki ndani ya ardhi ya Watanzania."

DCEA

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa DECA, Aretas Lyimo amesema kuwa,mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameweza kubaini mitandao ambayo ilikuwa inajishughulisha na dawa za viwandani ambazo zinajumuisha heroin na cocaine.

"Na hivi sasa hizo dawa zimepungua nchini, tatizo limekuwa kubwa sana kwa dawa aina ya bangi. Bangi imeonekana kuwa ni tatizo kubwa nchini Tanzania na inatumika na watu walio wengi kuliko dawa zingine za kulevya.

"Na inalimwa karibu mikoa yote nchini Tanzania,na hiyo operesheni tumeanza mikoa mbalimbali hapa nchini, ili kutokomeza zao la bangi hapa nchini,"amesema Kamishna Jenerali huyo.

Amesema, kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa wanataka kuanza kushirikiana na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusaidia kukomesha kilimo hicho, baada ya kuona vijana wengi, baada ya kukosa dawa za heroin na cocaine kwa sasa wameangukia katika bangi na mirungi.

"Na bangi ndiyo tatizo kubwa zaidi kuliko hata mirungi, na bangi ndiyo inasababisha madhara makubwa katika jamii, kuliko hata dawa nyingine za kulevya, na ndizo zinazotumiwa na vijana wengi.
"Kwa hiyo, sisi kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kupitia Mbio za Mwenge tutakuwa tunaendelea kufikisha ujumbe kwa vijana wote nchini kupitia Mbio za Mwenge.

"Lakini, pia tunaandaa mikakati mingine ya kuhakikisha kwamba operesheni zinaendelea nchi nzima hususani kwenye mikoa ile ambayo imekithiri kwa kilimo cha bangi,lakini na wilaya zile ambazo zina matumizi makubwa ya bangi.

"Lakini, pia tutashirikiana na viongozi wote wa Serikali kuanzia ngazi za vitongoji hadi mikoa ili kuhakikisha tatizo tunalipunguza na vijana waaachane na hiyo biashara ya bangi, matumizi ya bangi na biashara ya kilimo cha bangi.
"Ili tuhakikishe tunawaokoa vijana wetu kitaifa na vijana waanze kulima mazao mbadala, lakini pia tutashirikiana na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji baada ya kugundua kuwa, bangi nyingi inalimwa katika mabonde ya maji na watu wengi wanachepusha maji wanalimia bangi.

"Sasa tukishirikiana na hizi wizara tutahakikisha ili tatizo linaisha katika maeneo yote nchini, mmemsikia Mheshimiwa Rais akizungumzia mikoa ambayo ina matumizi makubwa ya bangi hapa nchini,tutahakikisha kwamba, hilo tatizo tunaliondoa hapa nchini kwa kupitia huo ushirikiano.

"Lakini, pia hivi karibuni tumeingia ushirikiano na TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa),tumeingia makubaliano na TAKUKURU, lakini pia tumezindua mwongozo wa uelimishaji na TAKUKURU ili kuhakikisha hii elimu inafika kwa wanafunzi wote kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu, lakini pia na nje ya mfumo wa elimu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news