MARRAKESH-Benki ya Dunia kupitia programu yake ya Ushirikiano katika Usimamizi na Utoaji wa Ushauri kuhusu Hifadhi ya Akiba ya Nchi (Reserve Advisory & Management Partnership {RAMP}) imekua ikishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kutoa mafunzo na ushauri juu ya masuala yanayohusu hifadhi ya akiba ya nchi.
Kupitia programu hizi, wafanyakazi wa Benki Kuu wamekuwa wakijengewa uwezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu hifadhi ya akiba ya nchi hususan katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta hiyo kwa njia ya mafunzo ya nadharia na vitendo ambayo hufanyika Washington - DC nchini Marekani.
Akizungumza katika kikao na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ushauri na Usimamizi wa Rasilimali kutoka Benki ya Dunia, Therese L. Couture, amesema Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kwa kuendelea kutoa mafunzo, ambapo imepanga kuendesha mafunzo yapatayo 27 kwa mwaka huu yatakayohusisha washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani.
Kwa upande wake, Gavana Tutuba ameishukuru Benki ya Dunia kwa msaada mkubwa wanaotoa kwa kuwapatia wafanyakazi wa BoT mafunzo hayo muhimu ya namna bora ya kutunza na kusimamia akiba ya nchi, ambapo yamekuwa yakiwajengea uwezo wafanyakazi hao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, Gavana Tutuba ametumia fursa hiyo kuiomba Benki ya Dunia kuongeza nafasi za washiriki kutoka Tanzania kufikia washiriki 15 kwa mwaka.
“Mwaka huu wafanyakazi wawili wamepata nafasi ya kuhudhuria mafunzo haya, kama ilivyokua mwaka jana. Hata hivyo, Benki Kuu imeajiri wafanyakazi wapya katika kitengo cha kuhifadhi akiba ya nchi. Wafanyakazi hawa wanatakiwa kujengewa uwezo kwa kubadilishana ujuzi na wafanyakazi kutoka Benki Kuu za nchi zingine na kujifunza namna ambavyo nchi hizo zinakabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusu masuala ya usimamizi wa akiba ya nchi,”alisema Gavana Tutuba.
Gavana Tutuba ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mafunzo kwa mwaka huu yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar, Oktoba 23-27, 2023. Ambapo amesisistiza kuwa, BoT kama mwenyeji itakuwa tayari kutoa ushirikiano stahiki katika kufanikisha mafunzo hayo.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, katika Mkutano wa Kundi la Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya ya Madola uliofanyika Marrakech, Morocco.
Vilevile, Gavana Tutuba, amehudhuria mkutano wa Kundi la Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya ya Madola (CCBG), ambao umefanyika Marrakech, Morocco, sambamba na mikutano ya kila mwaka ya IMF na Benki ya Dunia.
Mada kuu ya mwaka huu ilikuwa "Jukumu la Benki Kuu katika Kufadhili Utunzaji wa Mazingira na Kujenga Ustahimilivu Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi". Mjadala ulijikita katika hatua za kusaidia kuimarika hali ya hewa na kuhamasisha ufadhili wa utunzaji wa mazingira bila kuhatarisha jukumu la msingi la Benki Kuu, pamoja na kubadilishana uzoefu na mbinu bora katika kufanya mfumo wa fedha kuwa rafiki kwa mazingira.