DODOMA-Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa mishipa ya damu ya ubongo bila ya kufunua fuvu kwa kutumia mtambo maalum unaotumia teknolojia ya kisasa ya Angio Suit.
Huduma hiyo inatajwa kupunguza gharama za matibabu na muda wa kuuguza kidonda na muda wa daktari kufanya upasuaji.
Hayo yameelezwa Oktoba 2,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Alphonce Chandika amesema wameingia ushirikiano huo ili kuendana na azma ya serikali ya kufungua mipaka na kuruhusu kushirikiana na wataalamu kutoka nje ambao wapo mbele kwa teknolojia ya matibabu.
''Huduma hiyo inatarajia kuanza ndani ya mwaka mmoja kwa sababu vifaa vipo,ikiwemo Madaktari bingwa wapo katika mafunzo yanayotolewa kwa ushirikiano wa Madaktari kutoka nchini Japani,''amesema Dkt.Chandika
BMH Hospital imekuwa ikishirikiana vizuri na TOKUSHUKAI Medical Group katika tiba ya upandikizaji figo,baada ya mafanikio kuonekana wameanza kushirikiana katika uanzishwaji wa utoaji huduma ya upasuaji ubongo bila kufungua fuvu.
"Tunaishkuru serikali kwa kuruhusu ushirikiano na hospitali za nje katika utoaji huduma za Afya ambazo hazipo nchini hii itasaidia kuongeza utalii wa matibabu,"amesem Dkt. Chandika.
Pia amesema kuwa wajapani wametoa kifaa cha Anglesut ambacho hutumika katika upasuaji wa Ubongo bila kutumia fuvu.
"Tunawashkuru sana Profesa Akio Hydo ambaye ni bingwa mbobezi na mshauuri wa huduma za Upasuaji Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua fuvu kutoka Japan na wenzake kwa ushirikiano wanatoa BMH ili kuhakikisha huduma hiyo inaanza,"amesema Dkt.Chandika.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa ya Fahamu,Uti wa Mgongo na Ubongo kutoka BMH Henry Humba amesema tatizo la kiharusi ni kubwa na ni imani yao kuwa ndani ya mwaka mmoja huduma hiyo itaanza kutolewa.
"Kutumia teknolojia ya kisasa katika upasuaji wa Ubongo bila kufungua fuvu ina gharama nafuu kuliko mgonjwa kulazwa wodini,kwa sababu tiba hii inakwenda kuzibua mishipa ya Damu moja kwa moja,"amesema Dk.Humba.
Amesema huduma hiyo itaanza kutolewa katika hospitali ya Benjamin Mkapa ndani ya mwaka mmoja,baada ya Madaktari hao kupata Mafunzo.
"Vifaa vya utoaji tiba hiyo vipo,lakini hutumika katika matibabu ya moyo,tiba ya Upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu haiko sana kwa sababu wataalam ni wachache,tuko takribani 28 nchi nzima,"amesema Dkt. Humba.
Hata hivyo amesema kuwa serikali iko katika hatua za uanzishwaji wa vyumba vya stroke unit,ambapo serikali huwashirikisha Madaktari hao na kuongeza kuwa vyumba hivyo vitachangia kuongeza uharaka wa kuanzishwa kwa huduma hiyo.
Hospitali ya Benjamini Mkapa imeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma za kibingwa na huduma bobevu ili kubeba dhima ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wananchi wapate huduma iliyobora pasipo kusafiri kwenda nje kupata huduma ya matibabu.