DODOMA-Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Kati Christian Mbwasi amewaomba wazee wa kimila na Machifu nchini, kwa nafasi zao kupinga matumizi ya dawa za kulevya, ili kuiokoa jamii.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi hao kutoka Kanda ya Kati Dodoma na Kanda ya Pwani kwa Mkoa wa Morogoro pamoja na Zanzibar, aliposhiriki sherehe za kimila zilizofanyika viwanja vya machifu eneo la Bwibwi - Jedengwa mkoani Dodoma alipokuwa akitoa salamu za DCEA.

"Nyinyi ni viongozi wa jamii, tunaamini kwa kupitia sauti zenu ujumbe wetu utafika kwa haraka kuhusiana na kuitaka jamii kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya...hivyo tunaomba ushirikiano wenu katika hili, ili jamii iondokane na matumizi na ununuzi wa dawa za kulevya,"amesema Mbwasi.

Awali Mkurugenzi kutoka Taasisi ya Pick Foundation, Shiganga George amesema, taasisi hiyo inaunga mkono jitihada zinazoendelea kufanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kupitia Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, ambaye ameendelea kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika kutumia na kuuza dawa hizo.

Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mabaraza ya Wazee Tanzania
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Umoja wa Machifu Tanzania