PWANI-Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Dkt.Franklin Rwezimula amezipongeza taasisi mbambali za elimu ambazo zinashiriki Wiki ya Elimu ya Watu Wazima kwani zimekuwa na mchango chanya kwa jamii nchini.
Dkt.Rwezimula ametoa pongezi hizo Oktoba 12, 2023 baada ya kutembelea Maonesho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima yanayofanyika Kitaifa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
"Kwenye hii Wiki ya Maadhimisho ya Elimu ya Watu Wazima yenye kauli mbiu isemayo 'Kukuza uwezo wa kusoma na kuandika kwa Ulimwengu unaobadilika kujenga misingi ya jamii endelevu na yenye amani'.
"Nimepita kwenye mabanda mbalimbali, nimepita kwenye mabanda yanayohusiana na kutoa elimu hasa kutoka vyuo vikuu, Chuo Kikuu cha DUCE, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini na vyuo vingine vinatoa programu mbalimbali hasa zinazohusu elimu ya watu wazima.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan awaelekeza Wizara ya Elimu, kuandaa mpango maalum wa kuwarudisha vijana shuleni waweze kufaidika na fursa za masomo, na sasa vijana wengi wamerudi katika vituo mbalimbali nchini.
"Lakini, nimepita kwenye mabanda ambapo kuna wanufaika wa programu mbalimbali ambazo zimeanzishwa zinazohusu elimu ya watu wazima, kuna vikundi vya kina mama watu wazima ambao walikuwa hawajui kusoma, lakini kulingana na programu ambazo zimeandaliwa wameweza kusoma.
"Lakini, wameanzisha shughuli mbalimbali za kuongeza kipato, lakini siyo kwa watu wazima tu hata vijana, hasa wale akina dada ambao walikatisha masomo, lakini baadae ilianzishwa programu ambayo iliwarudisha shuleni waweze kusoma na kupata ujuzi."
Wakati huo huo, Dkt.Rwezimula ametoa wito kwa wananchi kuweza kufika katika maonesho hayo ambayo kilele chake ni Oktoba 13, 2023 ili waweze kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kujipatia bidhaa bora zinazotengenezwa na vikundi vya akina mama.
"Ni bidhaa nzuri, ambazo zimetumia malighafi asilia, tulionazo hapa nchini, nimepita kwenye banda moja, nimeambiwa kuna mama ametengeneza mkaa ambao umesaidia katika utunzaji wa mazingira,kwa hiyo wanasema ni rafiki kwa mazingira.
"Nimepita sehemu nyingine wanatengeneza sabuni, sehemu nyingine wanatengeneza juisi kwa kutumia malighafi ambazo zipo nchini, hiyo watanzania njooni mpate elimu, elimu haina mwisho,"ameongeza Katibu Mkuu huyo.
TEA
Wakati huo huo, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imejivunia kuwa na wanufaika zaidi ya 49,000 nchi nzima walionufaika na mafunzo ya kuongeza ujuzi yaliyoendeshwa na vyuo mbalimbali chini ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na mamlaka hiyo.
Afisa Habari wa Mradi wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), Bi. Eliafile Solla akizungumza katika maadhimisho hayo amesema kuwa,wengi wa wanufaika hao kwa sasa wamejiajiri na waliosalia wameajiriwa kutokana na mafunzo waliyoyapata.
“Kwa wale waliojiajiri wameendelea kukuza wigo wa ajira kwa kuendelea kuajiri watu wengine kwenye shughuli zao za kibiashara,”amesema Bi.Solla.
Mafunzo ya kuendeleza ujuzi yanayotolewa na vyuo mbalimbali vyenye ithibati kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yamejikita kwenye sekta sita za kipaumbele ambazo ni kilimo uchumi, uchukuzi, ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), nishati, utalii na huduma za ukarimu.
Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitekeleza programu na mipango mbalimbali ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kwa lengo la kuwa na Watanzania walioelimika na wenye uwezo wa kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.