HGWT yamrejesha nyumbani binti aliyekimbia kukeketwa nyumbani

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara limefanikiwa kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake katika Kijiji cha Machochwe wilayani humo,binti Sophia John.

Ni binti aliyekimbia kukeketwa kutoka nyumbani kwao tangu mwaka 2018 na kupewa hifadhi katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na shirika hilo.
Sophia amerejeshwa kwao Oktoba 8, 2023 ambapo alikuwa akipatiwa hifadhi katika kituo hicho kilichopo Mugumu akiwa ameendelezwa katika fani ya ushonaji na ujasiriamali huku akipewa cherehani itakayomsaidia kumuingizia kipato baada ya kukaa nje ya familia yao kwa miaka mitano.

Hatua hiyo ni kufuatia mazungumzo na makubaliano yaliyofanywa na uongozi wa Shirika la Hope chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly,viongozi wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Serengeti, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii na Wazazi wake kukubali kumpokea Sophia kwa taratibu za kisheria na kuahidi kutomkeketa binti yao.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly amesema kuwa, Sophia alikimbia ukeketaji mwaka 2018 ambapo alikimbilia Kituo cha Polisi Mugumu.

Ni kufuatia kaka yake kutoa amri akeketwe na ndipo Dawati la Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wilayani humo walipomchukua na kumpeleka katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama. ambacho hutoa hifadhi wa mabinti wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni.

"Baba yake Sophia ni Mchungaji alisafiri akaenda katika mafunzo ya kichungaji kwa siku nyingi, kaka yake Sophia pale nyumbani akatoa amri kwamba Sophia akeketwe, lakini Sophia alikuwa akifahamu madhara ya ukeketaji kutokana na kufundishwa shuleni,"amesema Rhobi na kuongeza kuwa.

"Alitoroka akaenda Kituo cha Polisi Mugumu akahifadhiwa na ndipo Ustawi ya Jamii na Maendeleo ya Jamii walipomchukua na kumleta katika Kituo cha Hope Mugumu ambacho hutoa hifadhi kwa mabinti wanaokimbia kukeketwa, ambapo tumekuwa naye kwa miaka mitano kabla ya kumpeleka tumekaa na wazazi wake tumeongea nao wamekubali kumpokea na kumsaidia vitenge na vitambaa atumie ujuzi wake kujipatia kipato kwani cherehani tumempa bure,"amesema Rhobi.
Rhobi ameongeza kuwa, Sophia alitoroka kwao akiwa ni Mwanafunzi wa darasa la sita lakini hakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika alipopokelewa kituoni hapo aliweza kuendelezwa kitaaluma na kufanikiwa kuhitimu darasa la Saba japo hakufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na elimu ya Sekondari kutokana na kushindwa kufaulu masomo yake kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa, kutokana na kushindwa kufaulu kujiunga na elimu ya sekondari, Shirika lilichukua jukumu la kumuendeleza katika fani ya ushonaji, ujasiriamali na pia kumfundisha elimu ya ukatili wa Kijinsia na stadi za maisha na akiwa kituoni hapo ameishi kwa upendo na ushirikiano mzuri na wenzake ambao wanapatiwa hifadhi kituoni hapo.

Sophia ameweza kujifunza mambo ya hedhi salama, haki za binadamu na kumjenga kujiamini katika maisha yake ambapo kwa sasa amerejeshwa nyumbani kwao akiwa na ujuzi mkubwa na kupewa cherehani akaendelee na ushonaji ili kumuingizia kipato na awe msaada kwa jamii na familia yao.
"Naendelea kutoa wito kwa Jamii, tusiwakekete Watoto wa kike, tuwasomeshe na kuwawekea mazingira wezeshi ya kutimiza ndoto zao. Ukeketaji ni mila yenye madhara iachwe lakini pia ndoa za utotoni hazifai. Jukumu la kudhibiti vitendo vya ukatili lifanywe na kila mmoja, Sophia alitengana na familia yake kwa kutokana na kutaka kukeketwa wazee wa mila tusaidie kupinga ukeketaji tukishirikiana na Serikali na wadau wote,"amesema Rhobi.

Kwa upande wake, Sophia John amesema kuwa analishukuru Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kumpokea na kumpa hifadhi kwa muda wote huo na kumuendeleza katika ushonaji, ujasiri, kumpa ushauri wa kisaikolojia, na elimu ya ukatili wa kijinsia ambapo amesema atakuwa balozi wa kupinga ukeketaji katika Jamii.
"Nilishukuru Jeshi la Polisi Serengeti kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii na Mkurugenzi wa Hope Rhobi Samwelly kwa umoja wao wa kuhakikisha kwamba sikeketwi. Nimekuwa katika Kituo hicho nikipatiwa huduma zote muhimu na msaada wa kiroho na pia nimepewa Cherehani kama nyenzo muhimu ya kunisaidia kujipatia kipato kwani,"

"Nafahamu kushona, huu ni mtaji mkubwa na pia ujuzi nilionao utanisaidia kupata kipato. Niombe Wazazi tusikekete mabinti bali tuwasomeshe waje kuwa msaada kwa jamii na taifa letu ukeketaji ni kosa kisheria tusiogope kuwafichua mbele ya vyombo vya sheria wanaokeketa kwani wanarudisha nyuma maendeleo na juhudi za Serikali kutokomeza mila hii mbaya," amesema Sophia.
John Mgendi Mwikwabe ni baba mzazi wa Sophia ambapo ameshukuru kurejesha kwa Sophia nyumbani huku akiwa na ujuzi katika fani ya ushonaji na ujasiriamali pamoja na maarifa ya stadi mbalimbali za maisha.

Pia, ameahidi kumpa Ushirikiano Mwanaye na kutomkeketa kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo kutokea damu wakati wa kukeketwa, madhara ya kisaikolojia, hatati ya kupata magonjwa ya kuambukiza na ameishauri Jamii kuweka Mkazo katika elimu kwa Watoto wa kike na kuachana na mila hiyo ambayo pia kisheria ni kosa.
Jesca Fabiani ni mkazi wa Machochwe amekipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuwa msaada mkubwa wilayani humo kwa kupinga ukeketaji, ndoa za utotoni, na aina mbalimbali za ukatili wa Kijinsia sambamba na kutoa elimu ya ukatili kwa jamii ambapo uelewa na mwamko wa Jamii kwa Sasa umezidi kuimarika katika kukabiliana na vitendo hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news