NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema kuwa, huduma ya pensheni na mafao kwa wastaafu wasio wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inatolewa bure na huwa haitozwi fedha yoyote.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 24, 2023 mkoani Morogoro na Mhasibu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, CPA Jenipher Joseph katika siku ya pili ya kongamano la wamiliki wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii lililoandaliwa na Wizara ya Fedha.
CPA Joseph alikuwa anawasilisha wasilisho lililoangazia juu ya mafao ya mirathi na pensheni, mafao na pensheni kwa wastaafu.
Amesema, lengo la Wizara ya Fedha ni kutoa huduma bora kwa wastaafu ndio maana inawalipa pensheni na mafao yao kwa wakati ili waendelee kufurahia maisha yao baada ya kustaafu.
"Wizara ya Fedha inawakumbusha wastaafu wote kuwa huduma ya mafao na pensheni inatolewa bure, hivyo wasikubali kutapeliwa, kwani wazee wengi wamekuwa wakitapeliwa jambo ambalo linapelekea kufariki kwa msongo wa mawazo.
“Wateja wetu wamekuwa wakitapeliwa sana, wamekuwa wakitapeliwa na watu ambao wanajifanya ni watumishi wetu, wanawapigia simu wanawaambia tunataka kukuhudumia,halafu wanawaambia wawatumie kiasi fulani cha fedha, jambo ambalo ni utapeli.
“Ndugu wanahabari tusaidieni kuwaambia wazee wetu kwamba,huduma hii ya mafao, huduma hii ya pensheni inatolewa bure kabisa,”amefafanua CPA Joseph.
Vile vile, amesema changamoto inayowakabili kwa sasa kama wizara ni kwamba wastaafu wengi hawajui ni wapi wanatakiwa kupeleka malalamiko yao.
Amesema, wizara inapokea malalamiko mengi ambayo yangetakiwa kupelekwa Hazina ama kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ukiwemo NSSF na PSSSF.
Mbali na hayo amesema,Serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kutoa huduma bora kwa wastaafu.
“Kwa hiyo kila siku wizara imekuwa ikitafakari ni namna gani itatoa huduma bora kwa wateja wetu, ikizingatiwa kuwa, wazee wetu wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu, hivyo ni wakati wao wa kukaa na kufurahia mafao yao.”
Amesema, katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari ili waweze kupata ufahamu juu ya namna ya kufuatilia mafao au pensheni zao na waweze kuzipata kama ilivyokusudiwa.
"Wizara ya Fedha kwa wale ambao wanalipwa na sisi, huduma zinatolewa bure, na kama mstaafu yeyote ana shida yoyote basi afike au awasiliane na ofisi ndogo za Hazina zilizopo mikoa yote nchini."