Jaji Kiongozi awataka majaji wapya wa Mahakama Kuu kuharakisha mashauri

TANGA-Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuharakisha utoaji wa hukumu ili wananchi wapate haki yao mapema.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (aliyeketi mbele) akiwasilisha mada katika Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Kiongozi ameyasema hayo Oktoba 20, 2023 wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na IJA, na yalifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mnamo tarehe 02 Oktoba, 2023 hapa IJA Lushoto.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji hao wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Wengine ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (wa pili kushoto), ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kulia), Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Awadh Mohamed (kwanza kushoto) na kwanza kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu.

Mhe. Siyani amesema kuwa Mahakama ya Tanzania haitarajii kuona Jaji au Hakimu anakaa na hukumu bila kuisoma kwa zaidi ya muda uliyowekwa kisheria.

“Msizalishe viporo vya hukumu wala nakala za maamuzi yenu. Dunia inakwenda kasi na watu wanataka haki ipatikane kwa haraka. Hatutarajii, hatutarajii, hatutarajii kabisa kuwa Jaji au Hakimu, akae na hukumu bila kuisoma kwa zaidi ya muda uliowekwa kisheria. Sambamba na kusoma hukumu zenu ni kutoa nakala zake kwa wadaawa,” amesema Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa hotuba wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania (hawapo pichani) katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), jana tarehe 20 Oktoba, 2023.

Pia Mhe. Siyani amewahimiza Majaji hao kufanya kazi kwa bidii kwani utamaduni wa sasa wa Mahakama ya Tanzania ni Majaji kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza mashauri mapema.

“Moja kati ya tamaduni iliyojengeka sasa hivi ni kufanya kazi kwa bidii. Nawaambia kweli tena bila kupepesa macho, wengi wa Majaji wenzenu mnaoenda kujiunga nao, hawalali. Wanafanya kazi usiku na mchana. Mchana wanasikiliza mashauri na usiku wanaandaa maamuzi.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa neno kwa Majaji wapya wakati wa kufunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji asiyeiga utamaduni huu, atatambulika haraka kuwa hachezi ngoma wanayocheza wenzake. Ninyi mkaige utamaduni huu na mtapimwa sio tu na Mahakama bali na watanzania wenyewe,” amesisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.

Aidha Jaji Kiongozi amewasihi Majaji hao kuwa wavumilivu kwani watakutana na ukosoaji wa kila aina watakapokuwa wanatimiza wajibu wao wa utoaji haki.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, jaji mpya wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa amesema kuwa mafunzo hayo yamewajengea msingi ambao utawasaidia katika kazi yao mpya ya Ujaji wa Mahakama Kuu.

“Tunawashukuru wawezeshaji, wametupa ujuzi na mtazamo kuhusu mambo mbalimbali ambayo yatatusaidia sana katika utendaji wetu wa kazi, tunaamini mafunzo haya yametujengea msingi ambao utamsaidia kila mmoja wetu kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa ufanisi mkubwa,” amesema Mhe. Jaji Longopa.

Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Ntuli Mwakahesya na Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro wamebainisha kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuzifahamu taratibu, sheria na utamaduni wa Mahakama ya Tanzania na wameahidi kuyafanyia kazi kwa haraka mashauri kama alivyosisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania (waliyosimama) wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji hao wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Katika Mafunzo haya, Mada mbalimbali ziliwasilishwa na wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania, Taasisi mbalimbali za Umma na za binafsi. Majaji hao wapya waliteuliwa na Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 3 Septemba, 2023 na kuapishwa tarehe 14 Septemba, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news