ARUSHA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imetembelea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na kuzitaka Taasisi za Umma na Binafsi zinazo daiwa na kituo hicho kulipa madeni yao ili Kituo hicho kiendeshe shughuli zake kwa ufanisi na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuvutia utalii wa mikutano nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe.Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) akiwa na baadhi wa Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo walipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) walipotembelea kituo hicho jijini Arusha kujionea kinavyotekeleza majukumu yake na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) alipotembelea AICC na kamati yake kujionea Kituo hicho kinavyotekeleza majukumu yake na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa kwanza kulia) akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (wa pili kulia) na baadhi wa Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo wakiangalia ukumbi wa Simba uliopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) walipotembelea kituo hicho jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru akiwaelezea Waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) walipotembelea majumba ya Kituo hicho yaliyopo eneo la uzunguni jijini Arusha walipotembelea kituo hicho na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na kuendeshwa na AICC.
Akizungumza katika kikao na menejimenti ya AICC, Mhe. Kawawa amezitaka taasisi za umma na zile za binafsi kuhakikisha zinalipa madeni wanayodaiwa na Kituo hicho ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi.
“Tumemsikia MD wa AICC, Bw. Mafuru akiongelea changamoto mbalimbali zinazoikabili AICC kuwa ni pamoja na madeni ambayo taasisi za umma na za binafsi zinadaiwa, naseme hivi, taasisi zote za umma na za binafsi zilipe madeni ya AICC, ili kituo kiweze kujiendesha kwa ufanisini, kuunga mkono harakati za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuvutia mikutano mikubwa nchini na kutoa mchango stahiki kwa pato la taifa,” alisema Mhe. Kawawa.
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Bw. Ephraim Mafuru alipowaelezea Waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, katika picha kushoto ni Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia mausala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AICC Balozi Begam Taj wakati wajumbe ya Kamati hiyo walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa pili kulia) akimsikiliza mmoja wa Wabunge na mjumbe wa kamati hiyo akiuliza swali kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru wakati wajumbe ya Kamati hiyo walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Kamati ya NUU Mhe. Vita Kawawa, (Mb.) (wa kwanza kulia) akiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (katikati) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (kushoto) wakimsiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Bw. Ephraim Mafuru hayupo pichani wakati Kamati hiyo ilipotembelea Kituo hicho jijini Arusha.
Amesema kwa AICC kufanya kazi kwa ufanisi ni lazima iondokane na hiyo changamoto ya madeni kwani kulipwa kwa madeni hayo kutaiwezesha kufanya kazi zake kwa tija na ufanisi na hivyo kupata matokeo chanya na kupongeza uendeshaji wa miradi ya maendeleo inayoendeshwa na kituo hicho jijini Arusha
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, (Mb.) ameishukuru Kamati ya NUU kwa kutembelea AICC na kuitaka Bodi ya AICC kuhakikisha inashughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo yakiwemo madeni ya taasisi mbalimbali ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe. Byabato amewataka AICC wapitie upya na kwa ukamilifu orodha ya madeni wanayodai na kuangalia namna bora ya kukusanya madeni hayo, kuwakumbusha kwa viambatisho na kuangalia mbinu mpya za namna ya kudai madeni hayo ikiwa ni pamoja na kuangalia kama utoaji wa "offer" za kulipa madeni hayo kama unaweza kusaidiwa kupunguzwa kwa madeni hayo.
“ pitieni upya madeni yenu, angalieni njia za kulazimishana pia kama itawezekana, muwe na mikakati mahususi ya wadeni na njia za kulipa madeni, kuna madhara kwa madeni hayo kuendelea kuonekana katika vitabu vyenu nadhani mnajua kuwa yanaweza sababisha mshindwe kukopesheka pale mtakapotaka kufanya hivyo katika taasisi za kimataifa,” alisisitiza Mhe. Byabato.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AICC, Balozi Begam Taj akizungumza kuwakaribisha Wajumbe wa Kamatiya NUU walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha.
Wajumbe wa Kamati ya NUU wakiangalia moja ya kumbi za Mikutano katika Kituo cha AICC walipotembelea Kituo hicho jijini Arusha.
Awali akizungumza katika kikao na Kamati ya NUU, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC Bw. Ephraim Mafuru amesema AICC inaandaa mkakati wa kipaumbele utakaoiwezesha AICC kutekeleza vipaumbele vyake ili iende na wakati na kuhimili ushindani wa soko la Diplomasia ya Mikutano.
Amesema AICC pamoja na kufanya shughuli zake katika mazingira ya ushindani, inakabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwemo madeni ya muda mrefu ambayo taasisi za serikali na za binafsi hazijailipa AICC kwa muda mrefu sasa.
“Kwa sasa AICC inatekeleza shughuli zake kwa kuitangaza nchi katika nyanja ya utalii wa mikutano na matukio na hivyo kuvutia mikutano mingi kuja nchini kwa kuwa vituo vya mikutano duniani hufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine ambao ni wanufaika wa moja kwa moja wageni wanapo kuja nchini kwa ajili ya mikutano,” alisema Bw. Mafuru.
Amesema AICC imeamua kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na kufanya mabadiliko yanayoendana na wakati kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Kituo wa mwaka 2022/2023-2026/2027 ulioidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi mwezi Juni 2022 na kuanza kutumika rasmi mwezi Julai 2022.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Saidi Shaib Mussa akizungumza katika kituo hicho ameipongeza Bodi na Menejimenti ya AICC kwa kutokufanya kazi kwa mazoea na kuwaahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na kufanya nao kazi bega kwa bega ili kufanikisha utendaji wao.
Kamati hiyo pia imekagua miradi mbalimbali ya uwekezaji ya nyumba za makazi, na hospitali na viwanja vya Kituo hicho na kuonyesha kuridhishwa na usimamizi na uendeshaji wa miradi hiyo.
Tags
Foreign Tanzania
Habari
Kamati ya Bunge
Kamati za Bunge
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)