LATRA kuanza kuwasajili Makondakta wa mabasi nchini

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI wa Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA),Bw. Johansen Kahatano amesema, mamlaka hiyo inatarajia kuanza usajili wa makondakta wa mabasi ikiwa ni hatua ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kuwahudumia abiria nchini.

Kahatano ameyabainisha yao Oktoba 19, 2023 katika kikao kazi kati ya LATRA na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, mafunzo kwa wahudumu hao yanakusudiwa kuanza kabla ya mwisho mwa mwezi huu wa Oktoba, lengo likiwa ni kuhakikisha wahudumu wa vyombo vinavyodhibitiwa na mamlaka wanafahamu sheria, kanuni na taratibu za usafiri ardhini.

"Ndiyo maana sasa kuanzia mwishoni mwa mwezi huu tunakwenda kuwasajili mpaka makondakta,tumeshaandaa hiyo mitaala tayari na mwishoni mwa mwezi huu mafunzo yataanza rasmi, akishapata mafunzo tunamsajili rasmi.

"Kwa hiyo sasa baada ya hapo hatutamtafuta mmiliki tuta-deal na kondakta huyo aliyewapakia hao watu kwenye gari kupita kiasi, madereva nao tunaendelea kuwasajili, kwa hiyo mfumo ukishakaa sawa kila mtu akawajibika, ninaamini hili litakwisha."

Amesema, wanaongeza ufanisi huo baada ya wao kama mamlaka kubaini kujirudia kwa makosa ya usalama barabarani huku wakiwajibika wamiliki wa mabasi na madereva peke yao.

"Baada ya kubaini haya makosa (usalama barabarani) yapo, tumechukua hatua kwa wamiliki wenyewe,tunaonya kwa mara ya kwanza, mara ya pili tunaweza tusichukue leseni yako, lakini tutakuny'ang'anya njia ambayo unatumia.

"Tumechafanya hivyo mara kadhaa.Na hii njia ya kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam, makosa hayo yapo mengi, Kigoma hasa na wengi tunawaondoa kwenye hiyo njia, tunakuwambia leseni yako hatukuny'ang'anyi lakini, Kigoma hautakwenda."

Vile vile, Kahatano amekiri mabasi kuendelea kukata tiketi za karatasi, "ni kweli wapo baadhi ya wamiliki na watu wao wanaokata tiketi za karatasi, sababu ni mbili ambazo tumezibaini, moja kuna hawa makondakta wanakuwa na nia ya kuwaibia tajiri wao.

"Kwa sababu ukikata tiketi kwenye mtandao itaonekana kuwa imepokelewa hilo la kwanza, la pili kuna hawa watu wanaitwa Masanange (wadaka abiria), kwamba gari lipo Magufuli (Magufuli Bus Terminal), lakini mita 200 kuna kibanda pale yaani hao wanaodaka abiria.

"Kwa hiyo ninamdaka abiria ninampa tiketi kabisa kupanda gari fulani, kwa hiyo huyo mtu unakuta ana tiketi zipatazo hata sita,kwa hiyo anakuja katika basi lako anasema abiria wangu huyu hapa,lakini nauli yake ni kiasi hiki.

"Yeye kachukua hela kubwa zaidi ya hiyo fedha, ukimkataza anampeleka kwa mtu mwingine tunawaita Masanange hao. Kwa hiyo, tunataka kwenda kujenga mfumo sasa ambao utaondoa mambo yote hayo, mifumo yote itawekwa kwenye mfumo wetu mmoja na abiria tokea nyumbani kwake atakua anaingia kwenye mfumo kujikatia tiketi yake.

"Mfumo ndiyo tunaenda kuujenga sasa baada ya kupata kibali, utakuwa na sura hiyo na utaondoa hilo tatizo, tena litakwisha kabisa."

Akizungumzia kuhusu madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani amesema kuwa, "Akizidisha speed hadi 90 au amechezea mfumo wa VTS tunapeleka namba ya gari na jina la dereva ili ashitakiwe, mwanzoni tulikuwa tunawaambia Polisi, gari namba fulani aje na mmiliki wake mchukue hatua, kwa hiyo mmiliki anakwenda pale polisi, ndiyo, lakini anampeleka day-worker, hapeleki dereva."

Mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button) unalenga kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo huo.

"Sasa hivi, kwa hii kitufe tunaandika namba ya gari, jina la dereva, namba yake ya leseni...kwa hiyo tum-suspect mtu ambaye ndiye anahusika, kwa hiyo hiyo imesaidia, kwa sababu hana namna ya kukimbia, tutampata tu."

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura 413 ili kudhibiti huduma za usafiri ardhini katika Sekta za Reli, Barabara na Waya. Sheria ya LATRA ilifuta Sheria Na. 9 ya mwaka 2001 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

LATRA ilianza kutekeleza rasmi majukumu yake tarehe 29 Aprili, 2019 baada ya Sheria yake kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 358 la tarehe 26 Aprili, 2019.

Aidha, LATRA inasimamia usafiri wa Barabara, Reli na Waya (Cable Car) ambapo kumekuwepo ongezeko la utoaji leseni za mabasi ya abiria (PSV), Malori (GCV), Magari Maalum ya kukodi (Special Hire), Pikipiki za Magurudumu Matatu (Bajaji), Pikipiki za Magurudumu Mawili (Bodaboda), Teksi Mtandao (Ride Hailing) na Teksi Kawaida (Cab).

Utekelezaji huo wa LATRA utaanza ikiwa tayari hadi kufikia Septemba 30, 2023 madereva 17,990 wameseajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya mamlaka hiyo.

Kati ya madereva hao, 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na mamlaka hiyo nchini huku miongoni mwao madereva wa mabasi wapatao 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho.

Katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news