NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo amesema, mamlaka hiyo ipo mbioni kutoa mwongozo kwa waendeshaji wa usafiri wa waya ambao wanatarajia uwekezaji huo utafanyika zaidi katika Sekta ya Utalii.
“Usafiri wa waya wenzetu wanautumia kwa ajili ya utalii, starehe na kuwahi maeneo ambayo yanaonekana kuwa na foleni.
“Kwa hiyo sisi tunachokwenda kufanya ni kuangalia ni namna gani ambavyo huu usafiri utakuwa na tija kwa hapa nchini hususani Sekta ya Utalii.
“Lengo ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuinua Sekta ya Utalii hapa nchini, sisi hatuwekezi huko bali, sisi tunaweka miongozo, kanuni za udhibti wa usafiri huo.”
CPA Suluo ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2023 katika kikao kazi baina ya LATRA na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, wadau wa LATRA ni wasafirishaji wa mabasi ya njia ndefu na mabasi ya miji na majiji, magari ya mizigo, madereva wa mabasi na malori.
Wakiwemo watoa huduma wa magari maalumu ya kukodi, watoa huduma wa teksi mtandao, abiria, taasisi za umma pamoja na wananchi kwa jumla.
Leo LATRA, ni taasisi ya 20 ambayo ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na wahariri wa vyombo vya habari ikiwa ni kutekeleza maono ya Msajili Nehemiah Mchechu.
Mchechu anasisitiza kuwa, suala la utawala bora katika mashirika haya ni jambo muhimu na ambalo halikwepeki, kwani lazima kila aliyeaminiwa awajibike kikamilifu ili mashirika hayo yaweze kuleta matokeo chanya.
Hivyo, kupitia vikao kazi hivi wanapata nafasi ya kuelezea wanafanya mambo gani, wanaelekea wapi na yapi matarajio ya mashirika hayo.
Aidha,mikutano hii imekuwa kiunganishi muhimu kati ya wahariri ambao kupitia vyombo vyao wanaueleza umma kile ambacho taasisi au mashirika yao wanakifanya.
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika ya umma, ndani ya hayo mashirika ya umma wana mashirika yenyewe, taasisi na kampuni ambapo zipo zaidi ya 298.
Aidha,miongoni mwa hizo kuna taasisi ambazo zinatoa huduma na zinafanya biashara huku nyingine zikijiendesha kibiashara, aidha kati ya hizo Serikali inamiliki hisa chache ambazo ni chini ya hisa asilimia 50.
Lengo la Serikali ni kuona mashirika hayo yanafikia lengo lake, ikizingatiwa kwamba yameanzishwa kwa mujibu wa sheria, mashirika haya kwa kiasi kikubwa yamefikia kiwango cha kuridhisha japo kuna machache ambayo hayajafikia malengo.
Mbali na hayo, CPA Suluo amesema, LATRA ni mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.
Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). “LATRA imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususani usafiri wa mizigo na abiria.”
Usafiri ambao unajumuisha mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu, usafiri wa reli na usafiri wa waya.
Amesema, malalamiko makubwa ambayo wanayapata mijini ni pamoja na daladala kukatisha ruti. Kutokana na changamoto hiyo, amesema wameweka namba maalumu ambazo abiria wakiona daladala inakatisha ruti au kufaulisha wawasiliane nao ili waweze kuchukua hatua za haraka.
Vile vile amesema, LATRA inawezesha matumizi ya teknolojia kama suluhisho kwa changamoto katika sekta ya usafiri.
Amesema, hayo yanafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya umma na sekta binafsi. CPA Habibu Suluo amesema, moja ya mafanikio yanayotambuliwa ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Mfumo huu umekuwa ukifanya kazi tangu mwaka 2017 na umeonesha matokeo chanya katika kuokoa maisha na mali.
“LATRA itaendelea kutumia teknolojia kutatua changamoto za usafiri nchini.” Pia, amesema, kazi za mamlaka zimeainishwa katika kifungu cha tano cha Sheria Na.3 ya LATRA ya mwaka 2019 ikiwemo kutekeleza majukumu ya Sheria za Kisekta.
Amesema, wanatoa leseni, kuhuisha leseni na kufuta leseni pale ambapo wanabaini mtoa huduma anahatarisha usalama wa wananchi.
“Lakini, hatujawahi kufuta leseni moja kwa moja.” Katika hatua nyingine, CPA Habibu Suluo amesema kuwa, “Sisi LATRA kazi yetu tunaona inaenda vizuri sana kutokana na uongozi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Kwa namna ya kipekee tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweka muundo mzuri wa uongozi ambao unatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.”
Amesema, mchango wa sekta binafsi katika Sekta ya Usafrishaji hapa nchini ni mkubwa, hivyo wataendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Majukumu mengine, CPA Habibu Suluo amesema ni kutoa, kuhuisha, au kufuta leseni za usafirishaji.
Amesema, kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kisekta, LATRA inawajibika kusimamia viwango vya ubora wa huduma na usalama katika sekta zinazodhibitiwa.
Aidha, CPA Habibu Suluo amesema, wanaratibu shughuli za usalama wa usafiri ardhini,kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini.
Jukumu linguine ni kuhakikisha na kuthibitisha hali ya usalama wa vyombo vya usafiri wa umma ardhini kwa matumizi.
“Kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia viwango vya uwekezaji, gharama, upatikanaji na ufanisi wa huduma.”
Wakati huo huo, CPA Habibu Suluo amesema wanashughulikia na kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko na kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa mamlaka.
“LATRA tunahudumia na kuwajali wadau wetu wote wanaotumia usafiri wa barabara pamoja na usafiri wa reli."