Madereva 17,990 wasajiliwa LATRA, haya ndiyo usiyoyafahamu kuhusu wao

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo amesema, hadi kufikia Septemba 30, 2023 madereva 17,990 wameseajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya mamlaka.

Amesema, kati ya madereva hao, 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na mamlaka hiyo nchini.

"Miongoni mwa madereva hawa, madereva wa mabasi wapatao 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button). Matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo wa VTS;

CPA Suluo ameyasema hayo Oktoba 19, 2023 katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema, mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ambayo imeiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.

"Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mazingira wezeshi anayotuwekea.

"Haya yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi kutokana na uongozi mahiri na madhubuti wa wasaidizi wake, ambapo hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameunda wizara mpya ya Uchukuzi na kuwateua Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), kuwa Waziri wa Uchukuzi,

"Mheshimiwa David Kihenzile (Mb) kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof. Godius W. Kahyarara, kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ally Posi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, miongozo yake inafanya kazi zetu inakuwa rahisi, hivyo tunaifanya kwa ubora,"amefafanua CPA Suluo.

Pia amesema kuwa, katika usafiri wa barabara, kwa kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kutoka leseni 230,253 hadi leseni 284,158 ikiwa ni sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

Amesema, kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)( b) cha Sheria ya LATRA,mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji.

"Hivyo, mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara. Leseni hizi hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. Leseni hizi hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa."

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura 413 ili kudhibiti huduma za usafiri ardhini katika Sekta za Reli, Barabara na Waya. Sheria ya LATRA ilifuta Sheria Na. 9 ya mwaka 2001 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

LATRA ilianza kutekeleza rasmi majukumu yake tarehe 29 Aprili, 2019 baada ya Sheria yake kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 358 la tarehe 26 Aprili, 2019.

Aidha, LATRA inasimamia usafiri wa Barabara, Reli na Waya (Cable Car) ambapo kumekuwepo ongezeko la utoaji leseni za mabasi ya abiria (PSV), Malori (GCV), Magari Maalum ya kukodi (Special Hire), Pikipiki za Magurudumu Matatu (Bajaji), Pikipiki za Magurudumu Mawili (Bodaboda), Teksi Mtandao (Ride Hailing) na Teksi Kawaida (Cab).

Alisema, pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji huduma, juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita zimechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa ufanisi wa utoaji huduma.

CPA Suluo amesema, mamlaka hiyo inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kiudhibiti (RRIMS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

Vile vile, amesema kuna Mfumo wa Tiketi Mtandao, Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo wa e-Mrejesho pamoja na Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST).

“Serikali imeboresha miundombinu ya barabara kila kona zikiwemo zile njia zinazolisha njia kuu (feeder roads), hali ambayo imepelekea kuwavutia watoa huduma kuwekeaa kwenye biashara ya usafirishaji,"amesema CPA Saluo.

Amesema, mamlaka hiyo imejenga mfumo wa TEHAMA unaojulikana kama Railway and Road Information Managemet System (RRIMS).

"Mfumo huu unatumika kwa ajili ya maombi ya leseni za usafirishaji pamoja na kazi zingine za usimamizi wa shughuli za kiudhibiti za mamlaka."

CPA Suluo amesema, mfumo huu umeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Nyingine ni Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma (Government Electronic Payment Gateway - GePG), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na nyinginezo.

"RRIMS imeunganishwa na mifumo ya wadau wengine kama vile watoa huduma wa tiketi mtandao. Lengo la kuunganisha mfumo huu na mifumo mingine ni kurahisisha utoaji huduma za mamlaka kwa wananchi."

Amesema, Mfumo wa RRIMS hutumika kutoa leseni za usafirishaji na unamwezesha mteja kufanya maombi kutokea mahali popote alipo.

"Maombi yote yanayowasilishwa yanafanyiwa kazi siku hiyo hiyo na kuhakikisha mwananchi anapata leseni chini ya saa 24.

"Aidha,mamlaka inaendelea kuboresha mfumo huu ili kuanza kutoa leseni za kielektroni na hivyo kuondoa hitaji la wateja kutembelea ofisi za mamlaka kwa ajili ya kufuata leseni,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.

Amebainisha kuwa, maboresho hayo yatakapokamilika yatasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza kwa kiwango kikubwa muda wa kupata huduma za leseni.

Vile vile, CPA Saluo, amesema katika kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali na Taasisi nyingine katika kipindi cha miaka mitatu, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23,mamlaka imeweza kuchangia silingi bilioni 14.21 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

“Mamlaka hupaswa kuchangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (Consolidated Fund) kwa mujibu wa Kifungu cha 11(3) cha Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348 (Public Finance Act, Cap. 348).

"Mamlaka hutakiwa kuchangia asilimia 70 ya fedha za ziada (surplus funds) kila mwisho wa mwaka wa fedha kwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 42 cha Sheria ya Bajeti, Sura ya 439."

"Katika kipindi cha miaka mitatu, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23,mamlaka imeweza kuchangia shilingi bilioni 14.21 katika Mfuko Mkuu wa Serikali,"ameongeza Mkurugenzi Mkuu huyo.

Wakati huo huo, CPA Suluo akizungumzia usafiri wa reli ameeleza kuwa, mamlaka, imeendelea kutoa mafunzo kazini kila mwaka kwa wafanyakazi muhimu wa usalama katika uendeshaji wa reli kwa TAZARA na TRC.

CPA Suluo amesema, lengo ni ili kuwaongezea ujuzi wa kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 LATRA imepanga kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo unazingatiwa katika usafiri wa reli.

“Mafunzo ya aina hii husaidia kuwajengea uwezo wafanyakazi hao muhimu kuzuia ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu.

"Tathmini inaonesha kwamba, makosa ya kibinadamu katika uendeshaji wa shughuli za reli huchangia zaidi ya asilimia ya 85 ya ajali zote za treni kwa TRC na TAZARA.

"Hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu,” amefafanua CPA Suluo.

Vilevile amesema, LATRA imeanza kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) tangu mwaka 2017 na hadi sasa, zaidi ya magari 9,420 yameunganishwa na mfumo huo.

Amesema,magari 7,620 yapo hai na yaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo huo. “Mfumo umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na mwendokasi, umepunguza madhara ya ajali zinazotokana na mwendokasi na umerahisisha uchunguzi wa ajali pale zinapotokea.”

CPA Suluo amesema, Mfumo wa Tiketi Mtandao umesaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli. "Na Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaopatikana ‘Play Store’ kwenye simu zote za Android na unamwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini.

"Na mamlaka inaendelea kuboresha huduma za mfumo huo ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari,"amesema.

Pia, amesema mamlaka pia imejiunga na inatumia Mfumo wa Serikali wa e-Mrejesho unapatikana kupitia kwa ajili ya kupokea malalamiko,mapendekezo,pongezi au maulizo.

Mkurugenzi Mkuu huto ametoa kwa wananchi kutumia mfumo huo kuwasilisha maoni yao ambayo yatafanyiwa kazi ndani ya siku 21.

Aidha, amesema LATRA inatumia Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST) kwa ajili ya kutangaza na kuchakata zabuni mbalimbali.

Kutokana na matumizi ya mfumo huo, CPA Suluo amewashauri wazabuni wajisajili kwenye mfumo huo ambao unapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kuweza kushiriki kwenye zabuni serikalini.

Aidha, amesema LATRA inajivunia kutekeleza dhana ya ushirikishaji wa wadau kwa vitendo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, LATRA ilifanya jumla ya mikutano ya wadau 36 ikiwemo mikutano tisa ya kupokea maoni.

Ni kuhusu mapitio ya nauli, mikutano sita ya mabadiliko ya kanuni, mikutano sita ya kutoa elimu kuhusu masuala kuidhibiti, mikutano saba ya kutunza mazingira na kuimarisha usalama wa usafiri ardhini.

Vile vile, CPA Suluo amesema,mamlaka ilifanya mikutano nane kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali kwenye usafiri wa barabara na reli.

Katika hatua nyingine, CPA Suluo amesema, huduma ya usafiri wa kukodi kwa njia ya mtandao imeendelea kukua kwa kasi kubwa tangu ilipoanza hapa nchini mwaka 2017.

Amesema, hadi sasa zipo kampuni 15 zilizopatiwa leseni na LATRA kwa ajili ya kutoa huduma za teksi mtandao.

"Mamlaka imepanga viwango vya nauli elekezi kwa ajili ya huduma hizi na inaendelea kuzisimamia. Katika mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya magari 3,523 yalipatiwa leseni kwa ajili ya kutoa huduma za teksi mtandao.

"Leseni hizo ziliongezeka kwa asilimia 16.9 ikilinganishwa na magari 3,013 yaliopewa leseni mwaka 2021/22. Huduma za teksi mtandao zimerahisisha usafiri kwenye miji mikubwa unaopatikana kwa gharama nafuu ikilinganishwa na usafiri mwingine wa teksi za kawaida,"amefafanua CPA Suluo.

Amesema, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 LATRA imejipanga kuhakikisha kuwa huduma bora na salama za usafiri ardhini zinawafikia wananchi, kuondoa kero na changamoto mbalimbali katika sekta.

"Hii ni katika kutekeleza maelekezo anayoyatoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kwa mara.

"Pia, mamlaka imejipanga kusimamia huduma za usafiri ardhini ambapo huduma za usafiri wa barabara na reli zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuwezesha Tanzania kufanya biashara na nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC)."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news