Makamu wa Rais azindua Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Ijangala wa Kilowati 360

NJOMBE-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 27, Oktoba 2023 amezindua rasmi Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Ijangala wa Kilowati 360 unaomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kusini Kati katika kijiji cha Masisiwe Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Dkt. Mpango ameelezea kufurahishwa kwake na uwepo wa Mradi, na kuwataka Wadau wengine kujitokeza kuwekeza kwenye miradi ya namna hiyo katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wa bei
nafuu.

"Mradi huu umegharimu takribani shilingi bilioni 3 milioni 841. Kiasi cha pesa hizo, milioni 997 zimefadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), pamoja na Benki ya Maendeleo (TIB) kutoa Dola za Kimarekani 850 kwa mkopo wenye riba nafuu." Alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amesema, umeme ni kichocheo cha maendeleo ya watu kwa kuwa bidhaa za mazao ya misitu, kilimo, ufugaji na uvuvi lazima zisindikwe kwa kutumia nishati ya uhakika na ya bei nafuu.

"Sasa ili tufike hapo, tunahitaji uwekezaji imara na katika uzalishaji, usafirishaji na nishati ya umeme katika maeneo ya uzalishaji na usindikaji wa bidhaa,”amesema Mhe. Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa Mradi wa Rumakali ili kuongeza
upatikanaji wa Umeme Wilayani Makete.

Akizungumza wakati wa Hafla hiyo. Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa, Wizara ya Nishati inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na Umeme kwa wakati na kuwa kwa Wilaya ya Makete wanakaribia kumaliza kupeleka umeme kwa vijiji vyote 98

"Tunategemea hadi kufika terehe 30/10/2023 tutakuwa tumepiga hatua Ili Megawati 80 zote za mradi wa Rusumo ziweze kuingia kwenye Gridi ya Taifa.

"Kupitia REA na TANESCO tunatekeleza miradi mbali mbali ya nishati ikiwemo miradi ya kuzalisha pamoja na kusafirisha umeme sio tu ndani ya nchi yetu lakini Kwa kuunganisha nchi nyingine zikiwemo Zambia, Kenya, Uganda, Burundi na Malawi," amesema Naibu Waziri Kapinga.

Awali, akizungumza katika hotuba yake kwa mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Dayosisi ya Kusini Kati, Askofu Wilson Sanga alieleza kuwa, Mradi ulianza rasmi kwa tafiti mbalimbali mwaka 2010, lakini ujenzi ulianza rasmi Machi 2021 kama shughuli ya kwanza ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited, kampuni iliyoanzishwa na Dayosisi na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria
za nchi.

“Kwa sasa mradi unazalisha umeme wa kilowati 360 na umeunganishwa na Gridi ya Taifa (National Grid) kwa kufuata makubaliano ya kimkataba kati ya TANESCO na Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited yaliyosainiwa Desemba 2020, kufuata fursa zilizopo kwenye chanzo ingawa kinaweza kutoa umeme wa hadi megawati 2, iwapo mitambo itaongezwa,"amesema Askofu Sanga.

Askofu Sanga amesema, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ruzuku na imeendelea kuchangia sehemu ya gharama za ujenzi ambapo jumla ya shilingi za kitanzania milioni 997.5 zimetolewa pamoja na mkopo nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB (Dola za Marekani 400,000) sawa na zaidi ya milioni 850 fedha za kitanzania.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Viongozi wa Kidini na wakazi wa Makete.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news