Mchango wa Serikali utoaji huduma za figo ni mkubwa-Prof.Janabi

DAR ES SALAAM-Serikali imeweka mchango mkubwa katika utoaji huduma za matibabu kwa wagonjwa wa figo katika ngazi mbalimbali nchini kuanzia kwenye kusomesha watalaamu, miundombinu na mashine za usafishaji damu hadi upandikizaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi alipokutana na wagonjwa wanaosafishwa figo na ndugu zao ili kujadiliana nao changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ili kutafuta ufumbuzi kwa pamoja.

Amesema Uongozi wa Hospitali umepokea maoni yao na kuahidi kufanyia kazi changamoto zilizobainishwa ili kuboresha zaidi hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa hao.

Prof. Janabi amesema MNH-Upanga ina jumla ya wagonjwa 367 wanaosafishwa figo ambapo kati yao 190 wanatumia bima, 163 ni wagonjwa wa kuchangia huduma ambao wanapaswa kuchangia shilingi 180,000 ila kutokana na changamoto za kifedha wengi wao wanalipa viwango tofauti ambavyo ni kati ya shilingi 150,000, shilingi 50,000 na wengine wanatibiwa kwa njia ya msamaha.

Hivyo, Serikali inafidia kiasi kilichosalia. Seti ya kumsafisha mgonjwa damu (dialysis kit) mwenye tatizo la figo mara moja sokoni inauzwa shilingi 189,500 na inatumika mara moja.

“Ukiacha tu malipo, bado Serikali kwa MNH ilinunua na kusimika mashine 53 toleo la kisasa namba 5,008 ambapo 42 zipo Upanga na 11 Mloganzila,"amesisitiza Prof.Janabi.

Prof. Janabi amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanakata bima ya afya kabla hawajaugua na kutunza afya zao ili wasiugue magonjwa yanayoweza kuepukika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news