Mgongolwa:Rais Dkt.Samia ametuheshimisha wakulima, tutamfanyia 'surprise'

IRINGA-Mkulima na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Joseph Mgongolwa amesema, kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuwaheshimisha wakulima hapa nchini, nao wanatarajiwa kumpa heshima kubwa kupitia jambo watakalolifanya hivi karibuni.

Mgongolwa ameyasema hayo leo wakati akizungumzia namna ambavyo wakulima akiwemo yeye wanavyoguswa na mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kuwa, mkulima anayafikia malengo yake ya kuzalisha kwa wingi nchini.

Amesema, miongoni mwa mambo muhimu ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuyafanya ni pamoja na kuwaagiza Wakala wa Mbegu nchini (ASA) kuzalisha mbegu zenye ubora kwa bei ambayo mkulima ataimudu.

"Mtakumbuka Rais wa Jamhuri ya Muungano akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora alisema, tayari ameshawaagiza ASA kuzalisha mbegu hizo kwa wingi na zenye ubora, huu ni uamuzi wa busara sana, na hekima kutoka kwa mkuu wetu wa nchi.

"Sisi wakulima, tunachukulia maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa ASA kuwa ni dira sahihi kwetu kwa ajili ya kupata utoshelevu wa mbegu ambazo zitatuwezesha kuzalisha mazao mengi ili kuweza kuhudumia soko la ndani, nje na kupata chakula cha uhakika,"amesema Mgopngolwa.

Hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Tabora, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alisema, lengo la kuwaagiza ASA kufanya hivyo ni kujidhatiti kuzalisha mbegu za mazao yote hapa nchini ili kuachana na utaratibu wa kuagiza kutoka nje.

Rais Dkt.Samia aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa Nzega katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Samora.

Vile vile, Rais Dkt.Samia alizindua rasmi ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo (ASA) lililopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Rais Samia alipongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya ASA na aliwataka kuendelea kuongeza tija ya uzalishaji wa mbegu kulingana na wingi wa soko.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe alisema kuwa, Serikali imefanya mapitio ya mipaka pamoja na usanifu wa kina ili kujenga miradi ya umwagiliaji mkoani Tabora itakayowawezesha wakulima kunufaika na kilimo cha umwagiliaji na kuongeza tija katika uzalishaji.

Mheshimiwa Waziri Bashe alitaja miradi hiyo kuwa ni wa Wendere, mradi wa umwagiliaji katika Kata ya Simbo pamoja na mingine.

‘’Baada ya kufanya mapitio ya mipaka tumeanza kufanya usanifu wa kina na kuanza mpango wa kujenga hekta 3000 za umwagiliaji katika Bonde la Wendere.

"Katika jimbo hili la Igunga na Igulamali tuna mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Kata ya Simbo hekta 700, mradi wa Mwamapuli hekta 3500.

"Tunaanza mradi wa Igurubi hekta 1800; na pia mradi wa Buhekela hekta 334 ambapo mradi huu unaendana na usanifu wa kina wa Bonde la Wendere lote ambalo mwaka ujao wa fedha tutaanza kujenga hekta 3000 katika eneo hilo,”amesema Mhe. Bashe.

Aidha, Serikali iko katika mkakati wa kutekeleza miradi ya umwagiliaji kutoka katika ziwa Victoria kwenda katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Tabora na Dodoma.

Mgongolwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia imefanya mambo makubwa katika Sekta ya Kilimo ikiwemo kupaisha bajeti ya wizara ili kuwezesha wakulima kufanya vema nchini.

"Wakati Kamati ya Taifa ya Mbegu (National Seed Committee) ikiendelea kuidhinisha matumizi ya aina mbalimbali za mbegu mpya za mazao ya kilimo ikiwemo mpunga,mahindi, chai, alizeti, karanga na mengineyo, Serikali nayo imeweka fedha nyingi,kama mtakumbuka bajeti ilipaa kutoka zaidi ya shilingi bilioni 200 hadi trilioni moja, hii ni hatua kubwa.

"Hivyo, lazima sisi wakulima, tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anafanya, hivyo hivi karibuni wakulima tutafanya jambo kubwa, kwa maana ya 'suprise' kwa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kama shukurani yetu kwake,"amefafanua Mgongolwa.

Pia, Mgongolwa ameswashauri vijana kuendelea kujikita kwa wingi katika Sekta ya Kilimo kwa kuwa, Serikali imeendelea kuboresha sekta hiyo kuanzia pembejeo, mbolea na mengineo ili waweze kupata tija.

"Utajiri upo shambani, ndiyo maana tunaona Serikali imeweka nguvu kubwa katika kuimarisha Sekta ya Kilimo ili sisi vijana na Watanzania kwa ujumla tuweze kuneemeka, kwa hiyo ni wakati wetu kwenda shambani kuzalisha sasa,"ameongeza Mgongolwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news