Mikataba ya Uwekezaji wa Bandari imezingatia maoni ya Watanzania-Rais Dkt.Samia

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, amesema, haikuwa rahisi kufikia makubaliano ya Mikataba ya Uwekezaji wa Bandari.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Godius Kahyarara wakitia saini Mkataba wa Nchi Mwenyeji baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai iliyowakilishwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Sultan Ahmed bin Sulayem kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.

Amesema,Serikali ilisikiliza na kufuatilia maoni na hoja za kila mtu, hivyo hakuna kundi au sauti ambayo imepuuzwa, ambapo Serikali iliunda jopo la wataalam kufuatilia maoni hayo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Oktoba 22, 2023 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, wakati wa utiaji saini mikataba baina ya Serikali na Kampuni ya DP World kwa ajili ya uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

“Hakuna kundi au sauti ambayo imepuuzwa kwa kuangalia hoja zote, kazi hiyo ilifanywa vizuri sana na wale ambao ni wataalamu wa masuala ya kodi za Serikali tuliwajumuisha. Lakini katika jambo jipya ni lazima kutokee maoni tofauti na hapa tulipofika ni sehemu ya yale yote ambayo watanzania wameyatoa.

“Bandari ni kiunganishi kati ya nchi yetu na mataifa mengine na hatua hii inakwenda kuongeza mapato ya Serikali na kuongeza ufanisi katika shughuli za kiuchumi. Tunaendelea kuwakaribisha wawekezaji zaidi katika Taifa letu.

“Na mikataba hii iliyosainiwa imezaliwa katika yale makubaliano ya awali, lakini pia ninalishukuru Bunge kwa kupitia Azimio na Baraza la Mawaziri kwa kuridhia na kuangazia sheria zote ikiwemo ile ya Manunuzi.

"Nimpongeza Waziri wa Uchukuzi,Profesa Mnyaa Mbarawa, timu ya majadiliano, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano wake maana kila wakati tulikuwa tunamgongea mlango na hata kumwambia go and check,”amesema Rais Dkt.Samia

Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewashukuru Watanzania wote waliotoa maoni kwani linapokuja jambo jipya ni lazima watu wawe na maoni tofauti huku akiwakaribisha wawekezaji zaidi kuja kuwekeza nchini.

“Mawazo ya wawekezaji wa ndani kupewa bandari ni mazuri na ya kizalendo, lakini yapo mbali na uhalisia. Katika kusaini mkataba huu, maslahi mapana ya nchi yamezingatia,” amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Kwa uapnde wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mkeli Mbossa​ amesema,uwekezaji huo wa Serikali kupitia TPA utaongeza ufanisi kwa huduma za meli na shehena, kupunguza muda kwa bandari katika kuchakata nyaraka.

Pia, amesema utaongeza mapato ya serikali, kupungua kwa udanganyifu, kuimarisha nafasi ya ushindani kwa bandari, kuongeza ajira na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kuja bandari ya Dar es salaam.

Aidha amesema kuwa muda wa usafirishaji wa mizigo kutoka Mashariki ya Mbali utapungua kutoka siku 30 hadi 15.


Mkurugenzi huyo amesema,wastani wa meli kukaa nangani ikisubiri huduma ni siku tano hadi 10 huku Bandari ya Mombasa ni siku 1.25 na Bandari ya Durban ikiwa ni wastani wa siku 1.6.

Amesema.mikataba inayosainiwa ni baina ya nchi mwenyeji, mkataba wa ukodishaji na uendeshaji wa gati namba 4-7 lakini pia kutakuwa na sehemu ambayo gati 0-3 zitaendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya TPA na kampuni ya DP World kwa shughuli za kibiashara na shughuli za kiserikali.

Amesema, mikataba hiyo, haihusishi eneo lote la bandari wala bandari zingine za Tanzania, ambapo kwa upande wa gati namba 8-11, mchakato wa kumpata mwendeshaji mwingine umeshaanza kufanyika na akipatikana mwekezaji mwingine mwenye sifa atakabidhiwa na sio DP World.

Hata hivyo amesema,mkataba huo utakuwa wa miaka 30 na utendaji kazi wa DPW utakuwa unapimwa kila baada ya miaka mitano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news