NA GODFREY NNKO
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB) imesema, tangu kuanzishwa kwake ukwasi wake umefikia zaidi ya shilingi trilioni 7.2 ambazo zimekwenda kwa wanufaika 750,000 nchini.
“Kwa wale ambao mnatazama hesabu za kibenki, ukwasi wa Bodi ya Mikopo, kihasibu, kifedha umefikia shilingi trilioni 7.2 huu ni uwekezaji uliofanyika kwa miaka 20 iliyopita ambazo zimekwenda kwa wanufaika 750,000.“
Hayo yamesemwa leo Oktoba 26, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa HESLB,Abdul-Razaq Badru katika kikao kazi kati ya bodi hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Kama hii investment isingekuwepo kungekuwa na upungufu mkubwa wa watenda kazi wenye ujuzi katika taaluma mbalimbali.”
Amesema, hadi kufikia Septemba, mwaka huu kuna kiasi cha mkopo ambacho kimekusanywa ambacho kinakadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.3 kutoka kwa wakopaji zaidi ya 230,000. Aidha, amesema kiasi cha shilingi bilioni 700 cha mikopo hiyo zimeiva, lakini hazijakusanywa.
“Tuna kazi ya kujenga utamaduni miongoni mwetu wa unapokopa basi unalipa, waajiri ni wakala wetu wakubwa, lakini bado waajiri fulani fulani hawawasilishi kwa wakati, na wengine wanawasilisha makato ambayo yana upungufu,”amefafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Pia, amesema wapo katika hatua za kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha ukusanyaji wa mikopo hiyo ikiwemo kuunganisha mifumo yao na hifadhi za jamii na Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiwemo kuendelea kutoa elimu.
“Kigezo cha kutoa mikopo ni uwezo mdogo kwa famila isiyokuwa na uwezo wa kulipa. Sisi kama jamii, hatufahamu kama hii scheme ya mkopo inasaidia kuongeza kiasi fulani ambacho umepungukiwa.”
“Serikali inafanya uwekezaji mkubwa sana katika rasilimali watu, hivyo kila mtu wakiwemo waajiri wanapaswa kuunga mkojo juhudi zetu za kuhakikisha wale ambao wamekopeshwa wanarejesha mikopo yao ili iweze kunufaisha wengine.”
Pia amesema, kwa sasa mifumo yao imeunganishwa na mifumo mama ya Taifa kwa ajili ya kuongeza ufanisi na utekelezaji wa majukumu yao.
Vile vile amesema, “kwa mwaka huu tuna wanufaika takribani 230,000 katika zile products tatu za under-graduate, diploma na Samia Scholar sasa hii ni namba kubwa ya wanufaika 250,000 ambao wanaguswa na fedha zilizopo.”
Pia, amesema Teknolojia ya Habani na Mawasiliano (TEHAMA) imeendelea kuwabeba katika kutoa huduma nchini.
Amesema, majukumu yao makuu ni kutoa mikopo na urejeshaji ambapo pamoja na miaka 20 ya taasisi, pia kuna juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali za kukusanya mikopo iliyoiva.
Akizungumzia kuhusu vikao kazi hivyo, Afisa Uhusiano na Mawasiiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri amesema kuwa, “Ofisi ya Msajini wa Hazina tunasimamia maslahi ya Serikali kwenye taasisi za umma, tunaamini kwamba mali ya Serikali ni mali ya umma.
"Kwa mashirika haya au hizi taasisi wadau wake wakubwa ni umma, umma unatarajia malengo ya kuanzishwa kwa taasisi na mashirika haya yaweze kutimia, kama wanatoa huduma iwe bora, kama wanafanya biashara basi iwe na faida kwa maslahi ya Taifa.”
Amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia kwa maono ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliona kuna changamoto kwa haya mashirika na taasisi kwamba yanafanya mambo mazuri, lakini hayafahamiki.
“Kwa hiyo fursa ya mikutano hii ni kuzikutanisha taasisi na mashirika ya umma yaweze kusema, malengo yao, mafanikio yao, changamoto zinazowakabali, walipotoka, walipo na wanapolekea.”
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa HESLB,Abdul-Razaq Badru amesema, kazi yao kubwa ni kusimamia rasilimali za Serikali, kupitia mikopo ambayo inawekezwa kuwezesha watu kusoma ili kupata watenda kazi bora.
“Sisi tunaamini kwamba, tunapojenga ushirikiano katika yale tunayoyafanya yanatuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea.”
Amesema, katika miaka michache iliyopita, wanafunzi wapya wameongezeka kutoka 50,000 kwenda 70,000 ikiwemo wanafunzi wanufaika kuongezeka kutoka 140,000 hadi 220,000.
Pia, amesema kuna ongezeko la mikopo kutoka shilingi bilioni 464 hadi shilingi bilioni 786, mwaka huu.
“Uchumi wa kati unahitaji vitu vingi moja wapo ni watu wenye ujuzi.Mikopo hii ni moja wapo ya uwekezaji wa Serikali katika umma katika kupata watenda kazi bora.”
Amesema, kwa miaka minne kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wapya kutoka 50,000 hadi 70,000.
“Kwa mwaka huu peke yake, shilingi bilioni 731 inapelekwa kusomesha wanafunzi wa shahada ya kwanza, na hizi ndiyo zitakazosomesha wanafunzi wote 200,000.
“Samia Scholar mwaka jana ilitengwa shilingi bilioni 3 na mwaka huu shilingi bilioni 6 ambapo zaidi ya wanafunzi 1000 wanasomeshwa, huku maeneo yenye kipaumbele na umuhimu ya kipekee yakipewa uzito.”
Mkurugenzi Mtendaji huyo akizungumzia kuhusu mikopo kwa wanafunzi wanaosomea programu mbalimbali nganzi ya diploma amesema, Serikali imetanga zaidi ya shilingi bilioni 48.
“Mikopo kwa wanafuzi watakaodahiliwa katika programu za dlpoma, kama hatua ya kwanza Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 48 ambazo zinatarajiwa kusomesha wanafunzi wanaoanza takribani 8,000,”amesema.