Mkahamasishe wananchi kulipa kodi, kudai risiti halali-Mwaipaja

NA GODFREY NNKO

WANAHABARI wa mitandao ya kijamii nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa Watanzania ili kuwa wazalendo katika kulipa kodi.
Sambamba na kila anayefanya manunuzi ya bidhaa kuhakikisha kuwa, anadai risiti halali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato yatakayoiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

“Lakini pia watu wajue umuhimu kwamba kuna masuala mengi ambayo yanatakiwa yafanyike, ninazungumzia suala la kodi kwa mfano,mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa sana ya kuhamasisha watu kulipa kodi.

“Lakini, kuongeza ile base ya walipa kodi, sasa hivi tunawalipa kodi wachache, kupitia misukumo yenu, mitazamo yenu, makala zenu, maoni yenu kwenda kuwauliza wadau kwamba kodi zina umuhimu gani, tunaamini kwamba ile base ya walipa kodi itaongezeka;

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja ameyasema hayo leo Oktoba 23, 2023 mkoani Morogoro wakati akifungua warsha ya siku mbili kati ya Wizara ya Fedha na baadhi ya wanamitandao ya kijamii nchini.

“Si hivyo tu, lakini pia tunataka watu zama hizi watu wawe wanadai risiti wanapofanya manunuzi yoyote na risiti zenyewe ziwe ni zile zenye thamani halisi ya hela uliotoa.

“Kwa mfano siku hizi watu wanaenda madukani, wanaulizwa unataka na risiti au hautaki na risiti, ikiwa risiti unambiwa Bwana nitakuuzia shilingi laki mbili, lakini bila risiti nitakuuzia laki moja na nusu.

“Kumbe ile simu bei yake ni laki na ishirini, au laki na nusu na hela nyingine ambayo ingesaidia maendeleo ya kwako wewe, kununulia dawa hospitalini, unamwachia mwenye duka.

“Kwa sababu mtu kakwambia ikiwa na VAT kiasi hiki, isipokuwa na VAT ni kiasi hiki, kwa hiyo maana yake tunaikosesha Serikali mapato yake ambayo yangetumika kuhudumia jamii, kutuhudumia sisi sote, kwa hiyo ninawasihi mtusaidie katika kampeni ya kuhamasisha wananchi kwanza walipe kodi, lakini pia wanapokwenda kununua kitu wadai risiti halali ya hela waliyotoa na wasikubali kwamba kuna risiti kiasi hiki, bila risiti kiasi hiki,”amefafanua Mwaipaja.

Amesema, mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuharabarisha umma kuhusu miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Serikali, hivyo wanapaswa kutoa taarifa sahihi ili umma ufahamu yanayofanyika.

“Na sisi (Wizara ya Fedha) tumeazimia kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi.”

Amesema kuwa, kupitia vyombo hivyo vya habari vya mitandaoni vimekuwa vinatoa taarifa kwa haraka na kwa kasi.

Mwaipaja amefafanua kuwa, Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na inaendelea ikiwemo ya kimkakati mijini na vijijini ambayo inapaswa kufahamika kwa jamii.

“Yapo mambo mengi ambayo Serikali inayafanya ambayo yanahitaji ninyi myaeleze, vivyo hivyo kuna mambo ambayo Serikali bado haijayafanya ambayo yanahitaji msukumo wenu kwa ajili ya kuyaeleza ili na sisi tuendelee kutafuta rasimali fedha kwa ajili ya kuyatekeleza.”

Aidha, amesema wanatarajia kukutana na wadau wengine wa mitandao ya kijamii kadri muda na rasilimali fedha zitakavyokaa vizuri.

Mwenyekiti wa warsha hiyo, Mathias Canal amewapongeza Wizara ya Fedha kwa kubuni na kuona umuhimu wa kuwakutanisha wanahabari kutoka mitandao ya kijamii.

Amesema kuwa,kwa sasa mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuufikia umma kwa haraka, hivyo wataendelea kushirikiana na Serikali ili kufikisha taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Kupitia warsha hiyo ya siku mbili la wanamitandao ya kijamii na Wizara ya Fedha, washiriki wanapitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo kufahamu muundo wa wizara.

Nyingine ni sheria mpya ya PPP,Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Mafao ya Mirathi na Pensheni, Mafao na Pensheni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news