Msigwa asisitiza kasi ujenzi jengo jipya la wizara Dodoma

NA ELEUTERI MANGI

KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amemtaka Mkandarasi anayejenga jengo jipya la wizara hiyo katika eneo la Mji wa Serikali, Mtumba ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) afanye kazi kwa saa 24 ili kazi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa ili watumishi waweze kuhamia katika ofisi hizo mapema Januari 2024 kama alivyoelekeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Aidha, amemtaka Mkandarasi anayejenga viwanja vya michezo na maeneo ya kupumzikia wananchi katika eneo la Nanenane jijini Dodoma aongeze nguvu kati na muda wa kufanya kazi ili kufidia muda aliopoteza ili kwenda na ratiba ya utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wa mkoa wa Dodoma na maeneo mengine nchini waweze kulitumia eneo hilo kwa shughuli za michezo na burudani.

Katibu Mkuu Gerson Msigwa ametoa maagizo hayo Oktoba 17, 2023 jijini Dodoma mara baada ya kukagua mradi ujenzi wa Ofisi za Wizara na eneo la Mradi wa ujenzi wa viwanja vya Michezo na kupumzikia.

“Nataka jengo hili likamilike kwa wakati, Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshatoa maelekezo majengo yote yanayojengwa Mji wa Serikali yaanze kutumika Januari 2024. Maagizo ya Waziri Mkuu kwangu ni maelekezo, yanapokuja maelekezo ya viongozi wangu nayapa kipaumbele kwanza kuyatekeleza,”amesisitiza Katibu Mkuu Bw. Msigwa.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshatoa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia kazi zinazokamilishwa hivyo Wakandarasi hao wanapaswa kuongeza nguvu katika eneo la mradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ujenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Haikamen Mlekio amesema, ujenzi wa ofisi hizo umefikia asikimia 69.4 akibainisha kuwa watafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa kazi hiyo vipo eneo la mradi na wanaendelea kupokea vifaa vichache ambayo navyo tayari vimeshaagizwa.

Akiwa katika mradi wa ujenzi viwanja vya michezo na maeneo ya kupuzikia wananchi la Nanenane, Katibu Mkuu Gerson Msigwa amemtaka Meneja Mradi Bw. Liang Li kutoka Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ambaye ndiye mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kwenda na ratiba ya kukamilisha ujenzi wa awamu zote tatu ndani ya miaka miwili iliyopangwa.

Kwa upande wake Meneja Mradi Bw. Liang Li amesema wao kama kampuni inayojenga mradi huo wamepokea maelekezo na watafanya kazi usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea kukamilisha kazi hiyo ambayo hadi sasa imefikia asilimia 12.

Mradi huo wa viwanja na eneo la kupumzikia unaojengwa Nanenane jijini Dodoma unahusisha viwanja viwili ya mpira wa miguu, netiboli, kikapu, majengo ya Utawala, bwawa la kuogelea, maeneo ya burudani pamoja na hosteli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news