Msilete nyaraka za kughushi, tutafunga uanachama-NHIF

DODOMA-Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewaonya baadhi ya wanachama wake wanaojihusisha na udanganyifu hususan wakati wa kuongeza wategemezi kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Uanachama Bw. Christopher Mapunda wakati akizungumza na Yaliyojiri NHIF ambapo amesema kumeibuka wimbi kubwa la wanachama kuwasilisha nyaraka za kughushi kwa lengo la kuongeza wategemezi ambao wako kinyume na utaratibu uliowekwa.

“Naomba nitumie fursa hii kuwaasa wanachama wetu kufuata taratibu zilizowekwa na Mfuko kwa kuwasilisha nyaraka zilizo sahihi za wategemezi, mfano vyeti vya kuzaliwa vya watoto na cheti cha ndoa. Tuna vielelezo vya kutosha juu ya suala hili, unamkuta mwanachama kawasilisha cheti cha ndoa na tukifuatilia unakuta mtu aliyefunga naye ndoa ni mama yake mdogo au shangazi na anafanya hivyo ili kutaka kuhalalisha kuwa ni mwenza wake, sasa tunaonya waache mara moja” alisema Bw. Mapunda.

Aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa na Mfuko kwa mwanachama anayebainika kuwasilisha nyaraka za kughushi ikiwa ni pamoja na kusitishiwa uanachama wake kwa muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja.

“Mfuko unapobaini viashiria vya udanganyifu una wajibu wa kujihakikishia nyaraka zinazowasilishwa kwa kuwasiliana na Mamlaka zingine za Serikali hivyo ili kuepuka usumbufu, kuchelewa kwa kitambulisho na kuchukuliwa hatua za kisheria basi mwanachama awasilishe nyaraka halali na kufuata utaratibu,” alisema Bw. Mapunda.

Akizungumzia muda wa utoaji wa vitambulisho, alisema kwa sasa, Mfuko unatoa vitambulisho kwa wanachama wake ndani ya muda wa siku saba kwa wanachama wanaojiunga kupitia mwajiri.

Aidha, kwa wanachama binafsi wanaojiunga kwa hiari kupitia utaratibu wa Vifurushi huanza kupata huduma siku 30 baada ya kujiunga hivyo hupewa vutambulisho baada ya muda huo.

Bw. Mapunda ametumia fursa hii kuwahamasisha wanachama kujiunga na huduma za Mfuko ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news