DAR ES SALAAM-Mtanzania aliyewahi kuwa mshauri wa Rais Michael Charles Chilufya Sata wa Zambia katika masuala mbalimbali ikiwemo uchumi, Mwinjilisti Alphonce Temba amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwahimiza DP World kuanza kazi hata ikiwezekana ndani ya wiki hii.
“Na tunatamani ndani ya wiki moja, DP World wawe ofisini, maana watu wanataka matokeo, kama ilivyo kocha wa Simba anasema anaangalia matokeo, anataka matokeo, mbwembwe zimepitwa na wakati.
“Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan sana kwa sababu hotuba yake imepokelewa kwa furaha sana na mataifa jirani ambayo yanatutegemea kupitia bandari;
Temba kwa nyakati aliwahi kuwa mshauri wa marehemu Rais Sata wakati wa uhai wake kipindi akiongoza Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Septemba 23,2011 hadi kifo chake Oktoba 28,2014.
“Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuthibitisha Serikali kuyafanyia kazi kubwa maoni ya Watanzania mbalimbali pamoja yakiwemo pia na maoni yangu na wageni, na si Tanzania tu.
“Huko nyuma mimi pamoja na delegation kutoka Malawi tulitoa maoni na tulifika mpaka Kwala kwa sababu walikuwa wanaona umuhimu, kama nilivyosema kwamba wanatoa mizigo mbalimbali yakiwemo mafuta kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwa hiyo walikuwa wakiona kulikuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa mizigo yao kufika katika miji ya Lilongwe na mingine iliyoko huko Malawi.
“Kwa sababu ya foleni iliyoko bandarini Dar es Salaam, lakini pia kasi ya utoaji mizigo katika meli, hilo ndiyo jambo la msingi kabisa,”amefafanua Mwinjilisti Temba.
Pongezi hizo zinakuja ikiwa hivi karibuni, Serikali imeingia mikataba ya miaka 30 na Kampuni ya DP World ya kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.
Mikataba hiyo mitatu ya uwekezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam iliyoingiwa ni Mkataba wa Nchi Mwenyeji, Mikataba ya Ukodishaji na Uendeshaji wa Gati Namba 4 hadi 7 za Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, Gati Namba 0 hadi 3 za Bandari ya Dar es Salaam zitatumiwa kwa pamoja baina ya Kampuni ya DP World na Serikali kupitia TPA kwa ajili ya shughuli zingine za kibiashara na Serikali.
“Na wageni wale walifika Kwala, walitoa dukuduku lao, walimuomba Mheshimiwa Rais,kwa kuwa wanamfahamu DP World kuanzia kule Beira na wanafahamu historia yao kwamba ni wachapa kazi, wana vifaa vya kisasa vinavyosaidia kushusha mizigo katika meli.
“Lakini, pia wamewazungumzia kwamba wana- connection ya kibiashara na wana ushawishi katika mataifa mengi duniani, wana meli zaidi ya 400 ambazo zinafanya kazi ya kusomba mizigo, kwa hiyo walikuwa wakiamini kwamba, Serikali ya Tanzania ifanye juu chini huu mkataba usainiwe.
“Safari hii nimepokea pongezi nyingi kutoka Malawi, wakimuheshimu na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, wameniomba nimfikishie salamu Wamalawi, Wazambia, Wakongo mpaka Wazimbabwe, tumekuwa delegations, simu nyingi nimepokea, tumekuwa tukizungumza, na tumefanya meeting conference, wamefurahi mno.
“Sasa hivi nimewashauri wafanyabiashara waji-organize huko waliko, waendelee kutoa information ili waendelee kujenga mahusiano mazuri na nchi yetu na bandari yetu, ili basi DP World wanapoanza kazi basi na wao mizigo yao waweze kuipitishia huku kwa urahisi.
“Na nimewaeleza wazi kuwa, kwa kuwa Serikali imejenga Bandari Kavu ya Kwala, nikawatia moyo kwamba kutakuwa na upendeleo mkubwa sana na unafuu mkubwa sana endapo wataendelea kuiamini na kuitumia bandari yetu.
“Lakini nikawaambia pia, kwa sababu hakutakuwa na foleni kubwa zaidi ya kilomita 100 kutoka pale mpaka Dar es Salaam, kwa sababu mizigo itashushwa Kwala basi kutakuwa na unafuu mkubwa sana wa kuchukua mizigo yao na kurudi nayo kwao.
“Kwa kweli makundi haya, Wamalawi, Wakongo, Wazambia na Wazimbabwe wamefurahi sana, na hata Watanzania wako Botswana ambapo na mimi niliishi Botswana wameonesha furaha kubwa na Watswana ambao wapo Kasane nchini Botswana karibu na mpakani na Zambia wamehamasika sana, kwani wanaona uamuzi wa hekima na busara uliofanywa na Mheshimiwa Rais.
“Mheshimiwa Rais, mwitikio ulioko nje ya nchi juu ya hotuba yako na wanachokitarajia kupitia uwekezaji wa bandari ni kikubwa sana.
“Ijulikane kwamba, umuhimu na mafanikio ya bandari yetu si kwa ajili yetu pekee, watu wengi wamekuwa wakizungumza, wamekuwa akishauri juu ya bandari.
“Lakini wamesahau kwamba bandari ni sehemu ya mataifa haya niliyoyataja pamoja na Uganda, Rwanda, Burundi, wale wanapofanya kazi kubwa ya kulerta mizigo yao kupitia bandari yetu ndipo tunafanikiwa.
“Kwa hiyo nimesimama katika eneo la Kimataifa au la nchi jirani, kuonesha furaha yao na wamenielekeza kabisa kwamba, wanatamani Mheshimiwa Rais alisikie hili.
“Walitamani kuonesha hisia zao kwa njia yoyote siku ile, walitamani hata kuja, hata kutuma sauti zao ili Mheshimiwa Rais ajue wamependezwa sana na hata kukaa kwenye vikundi vyao, kwenye taasisi zao kujadili, na karibuni kutakuwa na mkutano kwa ajili ya kujadiliana namna ambavyo wataweza kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kwa wingi kupitishia mizigo yao, kwa sababu wanamwamini Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Wanamuamini kwa sababu ya uongozi wake, wanamuamini kwa sababu wanajua hatawaangusha, wanamuamini kwa sababu Mheshimiwa Rais amesimamia suala hili.
“Wamempongeza sana Mheshimiwa Rais, wamewaomba Watanzania wampee muda, tena wanasema mpeni miezi sita tu, mtayaona mengi makubwa ambayo hamkuyajua.
“Mimi ninaleta salamu hizi Mheshimiwa Rais kwako kutoka kwa majirani zetu na mimi ninakuwa balozi wa kukusaidia Mheshimiwa Rais kuendelea kupiga kelele kwa mataifa haya, ambayo yote nimeyafika lakini pia, licha ya kufika huko nina connection kubwa na baadhi ya viongozi kwani nimekuwa mshauri wa marehemu Michael Sata alikuwa Rais wa Zambia.
“Kwa hiyo ninafahamika na watu wengi na wafanyabiashara, ninafahamika na nina delegation kubwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nimekwenda, ninafahamika.
“Kwa hiyo nitakuwa sehemu ya kupiga debe kama balozi, na Mheshimiwa Rais ikikupendeza nikupe ushauri mzuri pia, na sisi pia pamoja na DW World kuleta vifaa, kuleta mizigo, kutafuta masoko, lakini na sisi pia tuwe sehemu ya kuisaidia DP World.
“Ninalo wazo nzuri ambalo Mheshimiwa Rais kama litafanyika na Watanzania, ninaamini kabisa kwamba Bandari yetu ya Dar es Salaam, bandari ambayo itakwenda kufanya kazi ya kuleta mashehena ya mizigo mingi, tutapata fedha nyingi sana, hata hili deni la Taifa ninaona kabisa likikatwa zaidi ya nusu kwa sababu ya mafanikio ya bandari.
“Hivyo ninawatia moyo Watanzania, tusibabake bado nchi hii ni vumilivu, na bado mawazo na maono ya Mama ya bandari yetu ya Dar es Salaam kuwapa DP World ambao ninaamini ni watu sahihi wa kutusaidia, ndugu zangu inawezekana kuna Watanzania ambao hawajawahi kwenda kuchukua mizigo yao pale bandarini hata kontena moja, kontena moja lilikuwa linachukua siku ngapi, watanzania wangapi walikuwa wanalalamika vitu vinapotea.
“Magari yananyofolewa betri, magari mangapi yalikuwa yananyofolewa taa, watanzania wangapi walikuwa wanapiga kelele, leo tumekwishasahau hawa DP World hizo biashara za kupoteza vitu, sahauni, hazitakuwepo na wateja hawa wanaweza kubadilishiwa tairi, betri ikapotea kitu kidogo tu anahama, haleti mizigo yake, haleti gari yake.
“Show rooms za kule Zimbabwe, Congo, Zambia, Malawi, Zimbabwe zitaacha kuagiza magari pale vitu vidogovidogo vinapotea.
“Ndiyo maana wanapongeza kwamba, wanaijua DP World nimekaa Walvis Bay Namibia wanafanya kazi nzuri, na asilimia kubwa ya Watanzania wengi, pia walikuwa wakilalamika hawana exposure, hawana experience, hawana mfano walikuwa kwenye mkumbo, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Rais umeliona na tatizo limekwisha, labda niwashauri watanzania wenzangu tuwape sasa nafasi DP World wafanye kazi.
“Sisi sasa baada ya mwaka mmoja kama kuna shida tuanze kuiuliza Serikali, kwa sasa hivi tuiruhusu Serikali,”amefafanua Temba.
TPA
Hivi karibuni wakati wa utiaji saini mikataba hiyo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema mikataba itahusisha baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es Salaam na sio maeneo yote ya Bandari ya Dar es Salaam na mikataba hii haihusishi bandari nyingine za mwambao na maziwa.
“Mkataba huu una ukomo wa miaka 30 na utakuwa ukirejewa kila baada ya miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kurejea mpango wa uwekezaji,” amesema Mbossa.
Amesema pia kutakuwa na kampuni ya uendeshaji ambayo TPA itamiliki hisa, kuwekwa kwa viwango vya utendaji (key performance indicators), ambazo mwekezaji anapaswa kuvifikia.
Kwa upande wa watumishi wa sasa wa TPA, Mbossa amesema, wamepewa nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kwa mwekezaji.
“Jukumu la ulinzi na usalama katika eneo lote la bandari na yaliyokodishwa kwa Kampuni DP World yataendelea kubaki serikalini; mwekezaji atalipa kodi na tozo zote za serikali kwa kuzingaia sheria za Tanzania, “amesema.
Amesema, sheria za Tanzania zitatumika katika utekelezaji wa mikataba hii ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za Watanzania kushiriki katika uwekezaji huu kupitia vifungu vya sheria vinavyolinda maudhui ya ndani ya nchi ni haki ya serikali kujiondoa katika mikataba hiyo imezingatiwa.
Mbossa amesema, uwekezaji huo utakuwa na manufaa kwa serikali, ikiwemo ongezeko la ufanisi kwa huduma zitakazotolewa kwa meli na shehena hali itakayovutia meli nyingi zaidi na shehena kubwa ya mzigo itakayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam.
Pia uboreshaji wa huduma za bandari kwa kupunguza muda wa kuchakata nyaraka kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA ya Bandari itakayofungamanishwa na wadau wote wa bandari.
Nyingine ni kuongezeka kwa mapato ya Serikali hususan ya ushuru wa forodha kufuatia ongezeko la shehena na meli pamoja na udhibiti wa udanganyifu kupitia mifumo ya kisasa ya bandari ikakayofungamanishwa na mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia amesema kuiongezea uzoefu TPA na kuwajengea uwezo wafanyakazi na Watanzania katika uendeshaji wa bandari kwa viwango vya kimataifa, kuimarisha nafasi ya ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kikanda na kimataifa.
“Ajira kwa watumishi wa TPA na ajira mpya kwa Watanzania kufuatia kupanuka kwa wigo wa shughuli za uendeshaji wa bandari; kupungua kwa gharama za kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam;” amesema na kuongeza:
” Kuwepo kwa meli za moja kwa moja kutoka bara la Mashariki ya Kati kuja Tanzania ikilinganishwa na hivi sasa ambapo mizigo ya Tanzania huja kupitia nchi jirani;” amesema.
Pia manufaa mengine aliyotaja ni kuwa siku za kusafirisha mizigo kutoka Mashariki ya Kati na Mbali zitapungua kutoka siku 30 za sasa hadi siku zisizozidi 15.
Sambamba na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchukuzi kama vile reli na barabara kufuatia ongezeko la shehena linalotakiwa kusafirishwa kutoka bandarini kwenda sehemu nyingine.
Nyingine ni kuchagiza na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, usafirishaji wa madini pamoja na biashara.