Pato la Taifa linakuwa kwa kiwango cha kuridhisha-MPC

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu katika kutathmini mwenendo wa uchumi hapa nchini imebaini kuwa,Pato la Taifa kwa Tanzania Bara lilikua kwa kiwango cha kuridhisha cha asilimia 5.4 na asilimia 5.2 katika robo ya kwanza na ya pili, mtawalia na kuna matarajio ya kufikia makadirio ya ukuaji wa asilimia 5.3 kwa mwaka 2023.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba baada ya kamati kufanya mkutano wake wa 228 tarehe 27 Oktoba 2023.

Lengo la mkutano huo ulikuwa ni kutathmini utekelezaji wa Sera ya Fedha na mwenendo na mwelekeo wa uchumi.

Gavana Tutuba amefafanua kuwa, kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.2 katika robo ya kwanza ya 2023, na kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa asilimia 7.1 kwa mwaka 2023.

Aidha, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umepungua na kufikia asilimia 3.3 mwezi Septemba 2023, kutoka asilimia 3.6 mwezi Juni 2023, ukichangiwa na kupungua kwa bei za vyakula.

"Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 7.5 ukilinganisha na asilimia 6.5 mwezi Juni 2023,ukichangiwa na ongezeko la bei za vyakula.

"Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5, licha ya ongezeko la bei za mafuta hivi karibuni,"amefafanua Mwenyekiti wa MPC, Gavana Tutuba.

Wakati huo huo, MPC imebainisha kuwa, utekelezaji wa sera ya fedha, pamoja na sera thabiti za kibajeti, na kimfumo, zimesaidia kukabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei, kuchangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na uhimilivu wa sekta ya fedha nchini licha ya mtikisiko wa kiuchumi duniani.

Aidha, utekelezaji wa sera ya fedha pia umesaidia kupunguza shinikizo linalotokana na ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni nchini.

Kamati pia, ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2023 na kubaini kuwa, uchumi wa dunia bado haujaimarika licha ya ukuaji wa juu ya matarajio uliofikiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka. 

Mwenendo huu unatokana na kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani, migogoro ya kisiasa na ongezeko la bei za mafuta.

Mbali na hayo, kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi wa dunia na wa hapa nchini, Kamati ya Sera ya Fedha iliamua kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi katika uchumi.

Pia, amebainisha kuwa, Sera ya fedha itaendelea kutekelezwa sambamba na sera za kibajeti na kimuundo ili kufikia malengo ya kiuchumi.

Aidha,amesema utekelezaji wa Sera ya Fedha unalenga kuhakikisha malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya Extended Credit Facility (ECF) kwa robo inayoishia Desemba 2023 yanafikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news