NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo ameendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya elimu akishirikiana na wananchi jimboni humo ambapo amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kitongoji cha Gomora Kata ya Musanja ambao wameamua kujenga shule shikizi.
Lengo ni kuondoa tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda masomoni. Kitongoji cha Gomora ni moja ya vitongoji vitatu vya Kijiji cha Musanja, Kata ya Musanja.
Vitongoji hivi vitatu vinayo Shule ya Msingi moja iliyojengwa mwaka 1959 na Kanisa la Mennonite. Shule hiyo (S/M Musanja) kwa sasa ni ya Serikali.
Wananchi wa Kitongoji cha Gomora wamesema kuwa, wanafunzi walikuwa hawaendi shuleni na wengine wenye mahudhurio hafifu watasoma kwa ufanisi na kuhitimu masomo yao, huku wakimshukuru Prof. Muhongo kwa kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa mbinu shirikishi kati yake na wananchi pamoja na Serikali.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini imebainisha kwamba. "Matatizo makuu yanayowakabili wanafunzi wa S/M Musanja ni umbali mrefu wa kutembea kwenda masomoni,"
"Pia, mirundikano ya wanafunzi kwenye vyumba vya madarasa, uchakavu wa miundombinu ya shule iliyofunguliwa mwaka 1959.
"Kitongoji cha Gomora kimeamua kujenga Shule Shikizi.Ujenzi wa awali umekamalisha vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja ya walimu na choo chenye matundu sita."
Harambee ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, kwa kushirikiana na Kamati ya Siasa ya Wilaya (CCM) iliyofanyika Septemba 29,2023 ilikuwa ya mafanikio ya kuridhisha kwa kupata saruji mifuko 150.
"Ikiwemo 100 ya Mbunge wa Jimbo na 10 ya Diwani, shilingi milioni 3 za halmashauri yetu, fedha taslimu shilingi 306,000 zikiwemo shilingi 105,000 za walimu makada wa CCM na mchanga tripu 3 wana-Gomora waliahidi kuanza ujenzi na kweli wamefanya."
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa, kipaumbele cha kwanza jimboni humo ni elimu, vipaumbele vingine ni afya, kilimo, uvuvi, ufugaji, michezo na utamaduni. Huku wadau mbalimbali wakikaribishwa kuweza kuchangia ujenzi wa shule shikizi ya Gomora.