Prof.Muhongo azidi kuimarisha miundombinu ya elimu jimboni

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini wameendesha harambee kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maabara za Biolojia, Fikizia na Kemia za Shule ya Sekondari Nyanja iliyopo Kata ya Bwasi Wilaya Musoma Huku Prof. Muhongo akichangia mifuko 100 ya saruji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Oktoba 10, 2023, imebainisha kwamba harambee hiyo imefanyika Oktoba 9, 2023 Nyanja Sekondari kijijini Kome katika Kata ya Bwasi.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mapato ya harambee ni pamoja na fedha zilizopataikana shilingi 1,105,000, saruji Mifuko 14 ambapo mbunge Prof. Muhongo akitoa mifuko 100 ya saruji. Huku Kamati ya Ujenzi ya watu wanne imeundwa.

"Nyanja Sekondari ni ya Kata ya Bwasi yenye vijiji vitatu vyenye jumla ya vitongoji 23. Vijiji hivyo ni Bugunda, Bwasi na Bugunda. Sekondari hii ilifunguliwa mwaka 2006, na kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 547, na walimu 12 wenye ajira, na watano wa kujitolea.

"Sekondari haina maabara hata moja na mwitikio wa wanafunzi kusoma masomo ya sayansi ni mdogo sana Kwa mfano, Kidato cha Nne (Form IV) chenye jumla ya wanafunzi 96, ni wanafunzi 13 tu wanaosoma somo la Fizikia.

"Idadi ya Sekondari jimboni (kata 21) mwetu, Sekondari 25 za kata, Sekondari 2 za Binafsi, Sekondari 5 zinajengwa. Karibu tuchangie ujenzi wa maabara za masomo ya Sayansi kwenye Sekondari za Kata za Musoma Vijijini,"imeeleza taarifa hiyo.

Yohana Fabian na Jesca Paul ni wakazi wa Kijiji cha Kome Kata ya Bwasi wakizungumza kwa nyakati tofauti na DIRAMAKINI, wamepongeza jitihada za Mbunge wao anazoendelea kufanya kuimarisha sekta ya elimu jimboni humo hasa ujenzi wa maabara ambazo zitawaandaa wanafunzi kuja kuwa wana sayansi watakaosaidia kuleta maendeleo.

"Mbunge yupo bega kwa bega na viongozi wa chama (CCM) pamoja nasi wananchi na Serikali kwa ujumla akitushirikisha kuhakikisha tunalifanya Jimbo letu liwe la mfano katika maendeleo ya elimu, afya na sekta nyingine,"amesema Jesca na kuongeza kuwa,

"Harambee za ujenzi wa zahanati anazifanya vijijini mwetu, miundombinu ya elimu anachangia sana, na kila sekta anagusa Mungu azidi kumjalia afya njema aendelee kututumikia wana-Musoma Vijijini nasi tupo naye bega kwa bega mbunge wetu kuendelea kufanikisha agenda ya maendeleo jimboni mwetu,"amesema Jesca Paulo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news