Raia wazidi kutaabika, kupoteza matumaini Gaza

GAZA-Maelfu ya watu wameondoka majumbani mwao huko Gaza baada ya Jeshi la Israel kuwaonya zaidi ya watu milioni moja wanaoishi Kaskazini mwa Gaza na kuwataka kuhamia Kusini, hayo yakiwa ni kulingana na taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) leo Jumamosi.

Kabla ya onyo hilo, zaidi ya Wapalestina 400,000 walikuwa wakimbizi wa ndani, taarifa hiyo iliongeza. Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema kuwa limesambaza chakula kwa watu 135,000 katika makazi kote Gaza siku ya Ijumaa, lakini likaonya "vifaa vya kibinadamu vinapungua."

OCHA iliongeza kuwa watu wengi huko Gaza sasa hawana maji. "Kama suluhu la mwisho, watu wanatumia maji yenye chumvichumvi kutoka kwenye visima vya kilimo, na hivyo kusababisha wasiwasi mkubwa kuhusu kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na maji,"ilibainisha taarifa ya WFP.

Jeshi la Israel siku ya Ijumaa liliamuru watu milioni 1.1 wanaoishi Kaskazini mwa Gaza kuhama makwao, huku kukiwa na dalili kwamba, Israel inapanga kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Hamas kufuatia mashambulizi ya kundi hilo yaliyoua zaidi ya watu 1,300.

Kwa muda wa siku saba, ndege za kivita za Israel zimeshambulia Gaza kwa mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha mitaa na nyumba kuwa vifusi na kuua zaidi ya watu 1,900, wakiwemo watoto 614 na wanawake 370, na kuwajeruhi karibu wengine 7,700, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) pia limetangaza kuwa, halitahamisha shule zake ambako mamia kwa maelfu wamejihifadhi. Lakini lilihamisha makao yake makuu hadi Kusini mwa Gaza, kulingana na taarifa ya Msemaji wake, Juliette Touma.

Aidha, Philippe Lazzarini ambaye ni Kamishna Mkuu wa UNRWA, ameonya kwamba, "kiwango na kasi ya mzozo wa kibinadamu unaoendelea ni mbaya sana.Gaza inazidi kuwa shimo la kuzimu na iko ukingoni mwa kuporomoka," alisema.

Hata hivyo, alipoulizwa iwapo Jeshi la Israel litalinda hospitali, makao ya Umoja wa Mataifa na maeneo mengine ya raia, Msemaji wa Jeshi la Israel, Daniel Hagari alisema, jeshi litawaweka raia salama, "Kadiri tuwezavyo". Lakini alionya: "Ni eneo la vita." (IFP)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news