Rais Dkt.Samia awaonya vijana kuhusu dawa za kulevya

TABORA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaonya vijana wa Nzega na Tabora kwa ujumla kutojihusisha na matumizi wala biashara ya dawa za kulevya na badala yake waelekeze nguvu zao katika uzalishaji mali halali ili kujipatia kipato.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa wito huo Oktoba 17, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Nzega mkoani Tabora kwenye Uwanja wa Samora katika muendelezo wa ziara yake mkoani humo.

"Sasa hapa nizungumze na vijana wa Tabora, Serikali yenu inatumia fedha nyingi kujenga vyuo vya kuwafundisha, tunatumia fedha nyingi kuweka miradi ya umwagiliaji ili kilimo kikue.

"Tunatumia fedha nyingi kuleta mbolea na kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo ili vijana mjiingize huko, mfanye kazi mmpate mapato yenu halali.

"Lakini, vijana wangu Nzega mnanisikitisha nina taarifa kwamba, Serikali imefanya kosa kuleta barabara ya lami hii, kwa sababu sasa magari yanayopita na kudondosha dawa za kulevya yamekuwa mengi, na vijana wangu mnajiingiza huko.

"Nizungumze na ninyi vijana wangu, hii safari na huu uraibu mnaoingia hauiwafai na hautawapeleka pazuri, naomba sana Serikali ya mkoa, serikali za wilaya, Chama Cha Mapinduzi simamieni hili,vijana wetu waende kwenye maeneo ya kuzalisha.

"Wasijiingize kwenye majanga, hii si desturi wala si mila wala si historia ya Mkoa wa Tabora wala hapa mji wa Nzega. Niombe sana vijana wangu, nendeni kwenye maendeleo msiende kwenye mambo hayo, vijana wa hamasa hamasisheni wenzenu wasiende huko. Wafanye yenye maana wayaache hayo,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.

Wakati huo huo, Mheshimwia Rais Dkt.Samia amesema, ameshaiagiza Wakala wa Mbegu nchini (ASA) kuzalisha mbegu zenye ubora kwa bei ambayo mkulima ataimudu.

Rais Dkt. Samia amesema, lengo ni kujidhatiti kuzalisha mbegu za mazao yote hapa nchini ili kuachana na utaratibu wa kuagiza kutoka nje.

Awali Rais Samia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya ya Igunga ambacho kimegharimu shilingi bilioni 2.6.

Akihutubia wananchi wa Igunga katika mkutano wa hadhara, Rais Samia amesema, Chuo cha VETA ni muendelezo wa jitihada za serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ufundi itakayowasaidia kuajiriwa au kujiajiri.

Vile vile Rais Samia amesema serikali imeamua kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi stadi katika kila wilaya nchini na kuwa na chuo kikubwa kimoja katika kila mkoa.

Hali kadhalika, Rais Samia pia amesema serikali imedhamiria kukuza ujuzi wa vijana kwani ndio nguvu kazi ya taifa hivyo vyuo vya VETA vinajengwa ili ziungane na miradi na mipango inayoanzishwa na serikali ili kujenga uchumi wa nchi.

Rais Samia ameanza ziara ya kikazi mkoani Tabora ambapo alifungua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya mji wa Shelui, kupokea taarifa ya mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya 3 mzunguko wa 2 na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Iramba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news